Licha ya rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir kuahidi kuwa nchi yake isingerudi tena vitani, hali ya wasiwasi inazidi kutanda katika nchi hiyo.
"Mara kwa mara nimesisistiza kuwa nchi yetu haitorejea vitani,” alisisitiza kiongozi huyo Machi 8, 2025.
Hata hivyo, kuongezeka kwa kutoaminiana kati yake na Makamu wake Riek Machar kunaiweka nchi katika hatari ya kurejea katika mizozo ya ndani, kama ilivyoshuhudiwa kati ya mwaka 2013 na 2018.
Uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Sudan Kusini kuwakamata maafisa mbalimbali, akiwemo naibu mkuu wa jeshi na mawaziri wawili wanaomuunga mkono Machar, imezua mpasuko wa wazi.
Msemaji wa Serikali ya Sudan Kusini Michael Makuei, alishutumu maafisa hao kwa "kupingana na sheria".
Katika mkutano wao uliofanyika Machi 12, 2020 wakuu wa nchi za umoja wa IGAD, walitaka kuachiliwa kwa maofisa hao."
Jumuiya hiyo ilionesha wasiwasi wa kutokuaminia kati ya pande zinazohasimiana."
Kwa sasa, nchi hiyo ipo katika uongozi wa mpito kwa kuzingatia mpango wa 2018.
"Hii ni njia muafaka ya kuhakikisha serikali ya mpito inahitimishwa kupitia uchaguzi," alisema Alain Nyamitwe, mshauri mkuu wa masuala ya Afrika, katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Mkataba huu ulipelekea kuundwa kwa serikali ya mpito inayoongozwa na Rais Salva Kiir na kiongozi wa Sudan People’s Liberation Movement-in-Opposition (SPLM-IO), Riek Machar.
Serikali hiyo ilianza kazi yake mwaka 2020.
Makubaliano hayo ya amani yalisimamiwa na jumuiya ya IGAD na kufanikiwa kumaliza vita vilivyosababisha mauaji ya watu zaidi ya 400,000, huku mamilioni wengine wakiyahama makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Tishio la vita
"Ni vigumu kupata maendeleo kwa hali inavyoendelea kwa sasa nchini humo," Nyamitwe anaeleza.
Mzozo wa ndani ulioanza Desemba 2013, miaka miwili tu baada ya uhuru wa nchi hiyo, ulizorotesha maendeleo ya Sudan Kusini. Baadhi ya raia ya wa nchi hiyo walishindwa kujihusisha na shughuli za kibinadamu kutokana na kuyakimbia makazi yao.
Mnamo Machi 2025 Benki ya Dunia ilitoa Mfumo wa Ufuatiliaji Uchumi wa Sudan Kusini (SSEM) uliopewa jina la 'Njia ya Kushinda Mgogoro'.
Inabainisha kuwa "uchumi wa Sudan Kusini umeshuka kwa miaka mitano mfululizo" na inaonya zaidi kwamba uchumi unatarajiwa kupunguzwa kwa 30% katika mwaka wa fedha wa 2024/25.
“Kimsingi upungufu unatokana na kuvurugika kwa uzalishaji wa mafuta ambao umesababisha kupungua kwa mapato ya mauzo ya nje, yanayokadiriwa kufikia dola milioni 7 kwa siku. Hii imedhoofisha fedha za umma, ikichangia malimbikizo ya mishahara na kupunguza matumizi ya huduma muhimu kama vile afya na elimu,” Benki ya Dunia inaeleza.
Takriban 80% ya wakazi wa Sudan Kusini wanaripotiwa kukumbwa na mfumuko wa bei na uhaba mkubwa wa chakula. Utawala mbovu, usimamizi mbovu wa mapato ya mafuta, sera zisizo na tija za kifedha ndizo za kulaumiwa.
Kuwa na sekta hiyo ya kifedha isiyo imara pia inafanya kuwa vigumu kwa Sudan Kusini kupata mikopo ambayo inaweza kuwekezwa katika maendeleo.
"Sudan Kusini inaweza kuibua uwezo wa sekta yake binafsi na kufungua njia ya kupona na ustawi," alisema Charles Undeland, Meneja wa Benki ya Dunia nchini Sudan Kusini.
‘Kipindi cha mpito lazima kiishe wakati fulani’
Kulingana na Umoja wa Mataifa, Sudan Kusini ina takriban watu milioni 9.3 ambao wanahitaji msaada wa kibinadamu na mahitaji mengine.
Wengi wao ni wale walioathiriwa na mapigano ya awali ya Sudan Kusini, wengine walioathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa, wakati sasa idadi kubwa ya wale waliokuwa wamekimbilia nchi jirani ya Sudan kwa usalama wanalazimika kurejea huku mzozo wa ndani nchini Sudan tangu Aprili 2013 ukiwa umeng'oa mamilioni ya watu.
"Hatuwezi kuwa na Sudan iliyosambaratika na Sudan Kusini yenya mzozo, madhara yake ni makubwa" Nyamitwe anaelezea TRT Afrika.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM linasema kufikia Januari 2025 zaidi ya watu milioni moja walikuwa wamewasili Sudan Kusini, baada ya kukimbia vita nchini Sudan. Idadi hii imeongezeka huku mapigano ya ndani yakiendelea nchini Sudan.
Mzozo mwingine utakuwa mgumu sana kwa waliohamishwa na wale ambao hawajapata suluhu tangu mzozo uliopita.
Wataalamu wa utatuzi wa migogoro wanasema watu wa Sudan Kusini wanastahili kufanya uchaguzi na kuchagua viongozi wao, jambo ambalo linaweza kufanya makubwa katika kuzima mivutano hii inayotokana na ukosefu wa mfumo "imara" wa utawala.
"Kimantiki, hali ya sasa ni matokeo ya kuahirishwa mara nyingi kwa uchaguzi." Nyamitwe anaeleza.
Mnamo Septemba 2024 serikali ya mpito ya Sudan Kusini iliongeza mamlaka yake kwa mwingine hadi Februari 2027 na kurudisha nyuma ratiba ya kupiga kura hadi Desemba 2026 badala ya mpango wa awali wa Desemba 2024.
Huu ulikuwa ni muhula wa pili kuahirisha uchaguzi tangu serikali ya mpito kuanza kutekelezwa mwaka 2020.
Nicholas Haysom, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini aliutaja uamuzi huo kama "maendeleo ya kusikitisha kutokana na kuchanganyikiwa na uchovu wa watu wa Sudan Kusini kutokana na hali ya kupooza kisiasa na kutochukua hatua kwa viongozi wao kutekeleza makubaliano ya amani na kuleta mabadiliko ya kidemokrasia yaliyosubiriwa kwa muda mrefu."
Huku kukiibuka mvutano sasa kati ya watia saini wakuu wa serikali ya mpito rais Salva Kiir na makamu wake, Riek Machar, wataalamu wanasema suluhu la kudumu linalozingatia amani na mazungumzo ni muhimu.
"Kipindi cha mpito cha serikali lazima kiishe wakati fulani," Nyamitwe ameambia TRT Afrika.