Pengine wangeweza kuwa walinzi wa watu kama ilivyokuwa kusudio la uwepo wao nchini Kenya. La hasha; wanajeshi kutoka Kitengo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza Kenya (BATUK) wamegeuka kuwa kama nyoka wenye sumu kali kwa baadhi ya raia wanaoishi maeneo ya jirani ya kambi za wanajeshi hao.
Hata milio ya magari ya wanajeshi hao, imekuwa ni tishio kubwa kwa wananchi hao.
Kikosi cha BATUK kilikita kambi nchini Kenya kuanzia mwaka 1964, ambako wamegeuza sehemu ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kama eneo lao kufanyia mazoezi ya wiki nane kila mwaka, katika kambi mbili; ya Kifaru jijini Nairobi na ile ya Nyati, iliyoko katika kaunti ya Laikipia, kando ya Mlima Kenya.
Hata hivyo, nyuma ya mazoezi hayo, wanavijiji wa Samburu na Laikipia na maeneo yaliyo karibu na kambi zao, wamebeba majeraha; ya kimwili, kihisia na hata kijamii.
Shutuma dhidi ya BATUK
Wanajeshi hao wamekabiliwa na shutuma nyingi za nyakati mbaya kuanzia mauaji hadi uharibifu wa mazingira na hata ubakaji.
Wasichana na wanawake wanapokuwa wakihudumia mifugo, kufanya kazi zao za kila siku au kutafuta kuni, mara kwa mara wamekuwa wakivamiwa na wanajeshi hao wa Uingereza na kufanyiwa vitendo vya ukatili kama vile ubakaji, na uwepo wa watoto machotara katika maeneo hayo ni dhihirisho la madhila hayo.
Ubakaji
Zaidi ya kesi 1,000 za ubakaji uliofanywa na wanajeshi hao zimekisilizwa na kuchunguzwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Mmoja wa waathirika hao ni Ntilaren Supuko, mwanamke mwenye umri wa miaka 60 na mkazi wa eneo la Samburu.
Mama huyo anaisimulia TRT Afrika namna alivyoshambuliwa na wanajeshi hao, wakati akiwa anarudi nyumbani kwake.
“Walinikamata kwa nguvu, wakaanza kunishika, mmoja kwenye mkono huu na mwingine huu, mwingine akanipiga hapa (akiashiria ubavu wake). Nilianguka chini huku mwingine akanikaba shingo. Nilibakwa na wanajeshi saba kwa mpigo,” anaeleza kwa masikitiko.
Kulingana na Supuko, tukio hilo lilimnyang’anya heshima na utu wake, hali iliyosababisha atalikiwe na mume wake.
“Sehemu yangu ya kiuno kwenda chini imekwisha kabisa. Sijawahi kuwa kwenye mahusiano tena baada ya hapo….sina mtoto wa kiume, ni mimi na binti yangu tu.”
Kwa upande wake, Grace Supuko, binti ya Ntilaren, anasema analazimika kumnunulia dawa za kumpunguzia maumivu mama yake.
“Walau dawa hizo zinamsaidia kumpunguzia maumivu…ameenda hospitali nyingi na hakuna kinachoonekana, madaktari walisema hatojifungua tena aliharibiwa tumbo lake la uzazi, analia kila siku na hana amani hata kidogo,” anaeleza Grace.
Noldonyio Piro ni mwathirika mwingine aliyekuwa anaishi katika eneo la Samburu.
Anakumbuka namna alivyokumbwa na tukio la kutisha mwaka 1995.
Alikuwa akichunga mifugo ya baba yake, yeye na dada yake katika eneo la BATUK.
“Niliwaona watu weupe wawili sana. Hatukuwa tumewahi kuona watu kama wao hapo awali, mmoja alinitega na nilipoanguka, mmoja alinikanyaga mkononi na buti huku mwingine akanibaka.Huu mkono haufanyi kazi hasa hapa nilipokanyagwa. Ni tukio ambalo sipendi kulizungumzia,” anaeleza.
“Walibakwa kama wanyama, wakamkanyaga mke wangu mkono na miguu na mkono ukavunjika hali iliyomlazimu atibiwe kimila,” anaeleza Leko Piro, mume wa Noldonyio.
Tofauti na Ntilaren, Noldonyio ametafuta hifadhi kwa mume wake ambaye amekuwa kama faraja kwake kwa sasa.
Uzembe wa serikali na BATUK
Tangu mwaka 2004, viongozi wa jamii wamekuwa wakidai haki kwa waathirika wa madhila hayo bila mafanikio yoyote.
“Hakuna haki yoyote kwa akinamama hawa, wala hatujui kinachoendelea kati ya serikali ya Kenya na serikali ya Uingereza,” anasema Solomon Ole-Pussi, kiongozi wa jamii katika eneo la Laikipia.
Kutokana na aibu, waathirika wengi wameendelea kuwa kimya kwa hofu ya kutengwa na jamii, hasa miongoni mwa jamii ya Wasamburu nchini Kenya.
Kama ilivyokuwa nchini Kenya, wanajeshi wa Uingereza pia waliendesha mafunzo yao nchini Kupro, Canada na Ujerumani.
Tofauti na ilivyokuwa nchini Kenya, jeshi la Uingereza lilimewalipa fidia wakulima wa nchi hizo kutokana na matokeo ya uwepo wao katika maeneo hayo.
“Wana fursa ya kuchukua hatua kutoka kwa madai haya ili kuboresha uhusiano kati ya Kenya na Uingereza kutokana na mafunzo haya,” anasema Kelvin Kubai, wakili wa Mahakama Kuu ya nchini Kenya.
Watoto machotora
Wanajeshi hao pia wamehakikisha kuwa uwepo wao nchini Kenya hausahauliki.
Ongezeko la watoto machotara, waliotelekezwa ni dhihirisho la madhila yaliyofanywa na wanajeshi hao wa Uingereza.
“Naonekana tofauti sana na wengine; baba yangu ana ngozi nyeusi, ndiye aliyenilea, nataka tu kujua baba yangu halisi ni nani na kwanini aliniacha katika magumu haya,” anasema Louise Gitonga, mkazi wa Laikipia, Kenya.
“Hapa Kenya wamenipa jina la utani la ‘Muingereza’ na wanaponiita hivyo huwa najiuliza ninaishi dunia gani. Uingereza kwa upande mwingine haijui hata mimi nipo, achilia mbali uraia wangu,” anaeleza David Mwangi, kutoka Nanyuki, Kenya.
Akizungumza na TRT Afrika, Kamishna Tume ya Haki za Binadamu nchini Kenya (KNHCR), Profesa Marion Mutugi anasikitishwa sana na matukio hayo.
“Tunaamini kuna njama za kuhakikisha hakuna yoyote anayewajibishwa, lazima tuendelee kuwaaibisha, kuwaaibisha hao vijana wa Uingereza, na serikali ya Uingereza ijue ina wajibu kwa familia na akina mama walionajisiwa na watoto ambao ni watoto wa wanajeshi wa Uingereza na kwa mujibu wa sheria za Uingereza ni Waingereza.”
Kilio cha waathiriwa
Mume wa Noldnyio anakosa maneno ya kueleza uchungu wake.
“Tuliwaacha wale wanajeshi wa Uingereza mikononi mwa Mungu, tulimwachia Mungu awajibike kwa dhambi walizofanya.”
Lakini vipi kuhusu Ntilaren Supuko mwenye umri wa miaka 60? Tumaini lake ni nini?
“Sisi ni wanyonge, ni kama sisi ni vilema, kwanini wanakuja kutukandamiza, hawawezi tu kufanya kazi zao na kuondoka kwa amani, lazima watunyanyase? Au ni kwa sababu sisi ni watu weusi na wapumbavu, kama wanavyodai mara nyingi?’ Tunamlilia rais wetu William Ruto, achukue hatua na atusaidie. Hatuna uwezo hata kidogo.”
Kauli ya Uingereza
Kupitia majibu ya barua pepe, ubalozi wa Uingereza nchini Kenya unasema kuwa madai hayo yalionekana ya kawaida na yalikuwa na mtazamo wa jumla uliokaribia kuwa kama kauli za mazoea ambazo mashirika hutoa kila mara.
Majibu Yasiyotosheleza na mateso yasiyosahaulika
Walisema kuwa wanachukulia tuhuma zozote dhidi ya wanajeshi au wafanyi kazi wao kwa uzito, na kwamba hadi sasa wanaendelea kufanya uchunguzi mwingi kuhusiana na masuala haya, na matokeo yake yatashughulikiwa kwa ‘umakini wa hali ya juu’.
Mwisho wa ukimya: Haki itapatikana?
Milima ya maeneo ya Samburu na Nanyuki inaendelea kusitiri siri nyingi na maumivu mengi, Maelfu ya wanawake wamebeba maumivu kwa miaka mingi. Wengine wamekufa bila kusikika.
Lakini je, ni akina nani hasa hawa wanajeshi wa Uingereza waliohusika na unyama huu?
Na pia ni maafisa wakuu wapi serikalini wanaoficha utambulisho wao?