Kisa cha Yamoto Band na moto uliozimika ndani ya muda mfupi
Kisa cha Yamoto Band na moto uliozimika ndani ya muda mfupi
Kundi hili lilianza rasmi Septemba 21, 2014 wakati wakitumbuiza na kutambulisha wimbo wao mpya uitwao ‘Yamoto’, ndani ya uwanja wa burudani wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar es Salaam, Tanzania.
19 Machi 2025

Wamedumu kwa miaka mitatu tu.

Wanaitwa Yamoto Band, kundi la vijana wanne kutoka maeneo ya Temeke jijini Dar es Salam nchini Tanzania.

Kutana na Aslay, Marombosso, Beka Flavour na Enock Bella.

Kundi hili lilianza rasmi Septemba 21, 2014 wakati wakitumbuiza na kutambulisha wimbo wao mpya uitwao ‘Yamoto’, ndani ya uwanja wa burudani wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Haikuchukua muda kabla ya vijana hao waliojaaliwa sauti na uwezo wa kutunga na kucheza kukamata anga la burudani.

Kuanza kwa kishindo

Ndani ya mwaka mmoja, Yamoto Band, wakiwa bado wamoto, waliachia vibao vilivyokonga nyoyo ya mashabiki kama vile vile ‘Nitajuta’, ‘Niseme’, ‘Nisambazie Raha’, ‘Nitakupelepweta’ na nyingine kibao, wakiwa chini ya Saidi Fella, kupitia Mkubwa na Wanawe.

Vijana hawa hawakuchoka kutupa burudani, zikafuata nyimbo kama vile ‘Mama’, ‘Cheza kwa Madoido’, ‘Mpaka Nizikwe’ na nyingine nyingi.

Nyimbo hizo zikawapa nafasi ya kukwaa pipa na kwenda kimataifa, wakifanya ‘show’ za kutosha katika nchi mbalimbali zikiwemo Norway, Sweden, Uswisi, Denmark pamoja na Ujerumani.

Pia waliwahi kumshirikisha msanii Natacha kutoka Burundi katika wimbo ‘Unaniongopea’.

Kusambaratika

Hata hivyo, fununu za kuanza kuvunjika kwa Yamoto Band zilianza kuibuka mwaka 2017 huku Saidi Fella mwenyewe akiweka bayana kuwa Said Fella alitoa ufafanuzi kuwa kuendesha bendi imekuwa kazi kubwa hivyo umefika wakati kila mmoja kufanya kazi peke yake na wanapohitajika kwa pamoja watajikusanya.

Alianza kusikika Aslay akifanya ngoma zake peke yake, kisha akafuata Mbosso na Beka Flavor, na ndipo mashabiki wakathibitisha wenyewe kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa Yamoto Band, vijana waliotengeneza ‘chemistry’ ya ajabu wakiwa jukwaani.

Katika mahojiano yake na gazeti moja la nchini Tanzania, Beka Flavor alinukuliwa akisema kuwa walilazimika kujitenga kutokana na suala la maslahi akisisitiza kuwa kiasi walichokuwa wanakipata kama bendi, kilikuwa hakiwatoshi baada ya kugawana.

Na hapo ndipo wakakubaliana kuwa kila mmoja aanze kufanya kazi yake binafsi.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us