Serikali ya Rwanda imetoa taarifa kuelezea kuwa wananchi wa Ubelgiji bado wanaruhusiwa kuingia nchini Rwanda. Hii inafuatia kusitishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na Ubelgiji, Machi 17, 2025.
Rwanda imedai Ubelgiji ilitaka "kudhoofisha" maendeleo ya Rwanda kupitia "majaribio ya kusikitisha ya kuendeleza udanganyifu wake wa ukoloni mamboleo."
Imesema Ubelgiji imeamua kuiunga mkono Jamhuri ya Kidemokraia ya Congo, DRC kwa kuilaumu Rwanda kuwa inaunga mkono waasi wa M23 wanaofanya mashambulizi DRC.
“Kukatishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia hakutaathiri kwa vyovyote raia wa Ubelgiji wanaoishi Rwanda au wanaotaka kuzuru nchi hiyo,” taarifa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imesema.
Imesema raia hao bado watakuruhisiwa kuingi nchini bila viza.
“Wasafiri wa Ubelgiji bado wanaweza kupata viza baada ya kuwasili, bila ada ya viza kwa kukaa kwa siku 30, kwa mujibu wa sera ya viza inayotumika,” imeongezea.
Rwanda imesema ubalozi wake mjini Brussels umefunga milango yake na hautatoa tena huduma za kibalozi katika eneo la Ubelgiji.
Huduma za kibalozi zitatolewa na Ubalozi wa Rwanda nchini Uholanzi, mjini The Hague.