Jeshi la Sudan linakaribia kuchukua udhibiti wa Ikulu ya Rais mjini Khartoum kutoka kwa vikosi vya RSF, chombo cha habari cha serikali kiliripoti.
Hatua hii inakuja baada ya RSF kudhibiti ikulu na sehemu kubwa ya mji mkuu wa Khartoum baada ya kuzuka kwa vita kati ya Jeshi la Sudan na vikosi vya RSF mwezi Aprili 2023.
RSF, ambayo mapema mwaka huu iliunda serikali mbadala katika kongamano lililofanyika jijini Nairobi, inashikilia udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Khartoum na Omdurman, pamoja na magharibi mwa Sudan, ambako inapigania kuchukua udhibiti wa ngome ya mwisho ya jeshi huko Darfur, al-Fashir.
Kuchukuliwa kwa mji mkuu kunaweza kuharakisha utekaji kamili wa Sudan ya kati, kutoka kwa RSF. Hata hivyo pande zote mbili zimeapa kuendelea kupigania sehemu iliyobaki ya nchi, na hakuna juhudi zozote za mazungumzo ya amani zilizotekelezwa.
Janga la Kibinadamu
Wanajeshi wa Sudan na RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023 katika vita ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na wengine milioni 14 kuwa wakimbizi, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Utafiti kutoka vyuo vikuu vya Marekani, hata hivyo, unakadiria idadi ya vifo kuwa karibu 130,000.
Jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa inaendela kutoa wito wa kusitishwa kwa vita, ikionya juu ya hali mbaya kwa raia huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula.