Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, amenusurika kuuwawa siku ya Jumanne baada ya msafara wake kushambuliwa na magaidi wa al-Shabaab.
Kulingana na serikali ya Somalia, msafara wa Rais Mohamud ulikuwa unaelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu kabla ya kushambuliwa na magaidi hao.
Watu kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika shambulio hilo.
“Shambulizi hilo lilidhibitiwa na huku Rais akiwa salama salimini,” taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari ya Somalia imesema.
Kulingana na Wizara hiyo, shambulio hilo lilitokea katika wilaya ya Xamar-Jajab jijini Mogadishu.
Inadaiwa kuwa, msafara wa Mohamud ulikuwa unaelekea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu kuungana na vikosi vilivyo mstari wa mbele katika jimbo la Hirshabelle.
Vikosi vya usalama vimeanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo lililotokea katika sehemu yenye ulinzi mkubwa.
“Kwa umoja wetu na kuungwa mkono na washirika wetu wa kimataifa, tutafanikisha upatikanaji wa amani na utulivu wa kudumu nchini Somalia,” ilisema wizara hiyo.
Kikundi cha kigaidi cha al-Shabaab kimekiri kuhusika na tukio hilo.