Serikali ya kijeshi ya Niger imetangaza kujiondoa katika kundi la kimataifa la mataifa yanayozungumza Kifaransa liitwalo Organization Internationale de la Francophonie (OIF).
"Serikali ya Niger imeamua kwa mamlaka yake kujiondoa katika Jumuiya ya Kimataifa ya wanaozungumza Kifaransa," Laouali Labo, katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger, alisema katika taarifa yake Jumatatu.
Niger, koloni la zamani la Ufaransa chini ya utawala wa kijeshi tangu mapinduzi ya Julai 2023, imesitisha uhusiano wote wa kidiplomasia na wa kijeshi na Ufaransa, ikimtuhumu mtawala wake wa zamani wa kikoloni kwa kuunga mkono ukosefu wa utulivu nchini humo.
Serikali pia ilibadilisha majina ya mitaa na majengo katika mji mkuu wa Niamey, mwezi Oktoba.
Nchi hiyo inajiondoa katika OIF wakati ambapo shirika hilo lenye mataifa 88, lililoanzishwa Machi 1970 nchini Niger, linaadhimisha Wiki ya Lugha ya Kifaransa na Wiki ya Kifaransa.
Niger ilisimamishwa kutoka kwa shirika hilo kufuatia mapinduzi.
Baraza la Kudumu la Francophonie (CPF), lililokutana katika kikao kisicho cha kawaida mnamo Disemba 2023, lilitangaza kusimamishwa kwa Niger.
CPF ilidai kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum, ambaye bado anazuiliwa, na familia yake na wanachama wa serikali.
Pia lilitaka kurejeshwa kwa haraka kwa utaratibu wa kikatiba.