Mashindano ya Safari Rally Kenya, yanavyogeuka kuwa kivutio kwa watalii
Mashindano ya Safari Rally Kenya, yanavyogeuka kuwa kivutio kwa watalii
Mbio za magari maarufu World Rally Championship zimepangwa kufanyika katika mji wa Naivasha kuanzia Machi 20 hadi 23, 2025.
20 Machi 2025

Ni ile wikiendi ambayo mtu akiaga nyumbani kwenda dukani, basi ujue harudi tena nyumbani mpaka Jumatatu inayofuatia. Hii ni kwa sababu ya mashindano ya Safari Rally yanayoanza wiki hii huko nchini Kenya.

Mbio hizi za magari maarufu kama ‘World Rally Championship’ zimepangwa kufanyika katika mji wa Naivasha kati ya Machi 20 hadi 23, 2025.

Ni wakati wa msisimko hasa kwa wale wanaopenda kushuhudia mbio za magari na madereva wa kimataifa wanaonga’nga’nia nafasi za ubingwa.

Lakini pia ni wakati muafaka kwa Kenya kuuza utalii wake kwani, mashindano haya yanarushwa moja kwa moja kupitia runinga na mitandao ya kijamii na kutazamwa katika nchi zaidi ya 15 duniani.

Siku chache kabla ya mashindano kuanza, tayari mashabiki kutoka nchi mbalimbali kama vile Malawi, Afrika Kusini, Tanzania na Uganda wanaripotiwa kuvuka mipaka ili kushuhudia mashindano hayo.

Kwa kawaida mashindano hayo huanza katika mji wa Nairobi ambao ni mji pekee duniani ulio na Hifadhi ya Wanyama.

Tayari madereva wa kimataifa wa mbio za magari wameanza kutembelea Hifadhi ya Taifa
ya Nairobi na maeneo mengine kuionesha dunia mandhari ya Kenya.

Katika mji wa Naivasha, kuanzia Machi 20 hadi 23, miungurumo ya magari, vumbi na shangwe zitakuwa sehemu ya furaha kwa mashabiki, huku hoteli za viwango vyote zikiripotiwa kujaa.

Hata wale wanaotoa huduma za nyumba binafsi yaani ‘Airbnb’, wanasema kuwa wameishiwa nafasi vyumbani mwao. Kuna wale wanaotoa huduma za mahema kwa watu kulala sehemu za wazi. Lakini kuna wale ambao wanaaamini kuwa hupaswi kufunga jicho ukiwa Naivasha.

Huduma za viburudisho kama vile ma DJ, kampuni za vinywaji na vyakula tayari zimekita kambi mjini Naivasha kutoa huduma zao.

Kutoka maeneo ya Mto Elementaita na Mto Naivasha, maeneo maarufu kwa Heroe, viboko na wanyama wengine kama tembo, nyati, swala, twiga, ndivyo vitakavyotia nakshi mashindano hayo.

Halafu madereva kuingia katika mandhari ya kijani kibichi kabla ya kubadilika hadi tambarare na baadaye kupita sehemu za jotoardhi za Olkaria, na hatimae kuingia katika eneo la mchanga wa kina ambao utapima nguvu za gari na stamina ya dereva.

Madereva watapita katika milima yenye wanyama pori. Mashindano haya yatamalizikia katika eneo maarufu la "Hells Gate."

Ni hapa ndipo mashabiki hungoja kuwaona madereva wakipambana katika barabara ambazo hazijanyooka, eneo ambalo wataalamu wa rally wanasema hupima ubora wa dereva.

Matope, mawe, maeneo yenye kina kirefu, tishio la mvua za mara kwa mara na vivuko vya maji, huifanya Safari Rally Kenya kuwa kipimo cha uvumilivu kwa madereva, japo hili ndilo lenye kunogesha tukio hili.

Kulingana na serikali ya Kenya, takriban watu laki moja walihudhuria mbio hizo kwa mwaka 2024, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka mwaka huu.

Kulingana na sifa zote hizo, kama hujashuhudia Safari Rally, basi jitahidi mwaka huu usikupite. Usiwe mtu wa kila siku kusimuliwa habari za Vasha.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us