Ilikuwa furaha kubwa kwa tasnia ya filamu Tanzania, baada ya filamu ya Wa Milele? kutwaa tuzo muhimu kwenye Tuzo za Africa Magic Viewers Choice (AMVCA), zilizofanyika Mei 9, 2025.
Kwa sasa, gumzo kubwa Afrika Mashariki na barani Afrika kwa ujumla, ni filamu ya Wa Milele?, ambayo imeibuka mshindi wa kipengele cha ‘Kipindi Bora cha Maisha Halisia’ katika tuzo za Africa Magic Viewers Choice (AMVCA), zilizofanyika jijini Lagos, Nigeria.
Hii ni kwa sababu, filamu hiyo imetwaa tuzo hiyo, wakati ikiwa bado kwenye msimu wake wa kwanza.
Vile vile, imeshinda tuzo hiyo baada ya kuzishinda filamu nyingine kali barani Afrika, hasa za kutokea upande wa Afrika Magharibi, zikiwemo Ebuka, The Skillers na Amaka Taste Palm Wine.
Yote tisa, kumi ni kwamba, Wa Milele? imebeba tuzo katika kipengele cha ‘Kipindi Bora cha Maisha Halisia’.
Filamu hiyo inawaleta pamoja wapendanao nane, chini ya nyumba moja kwa kipindi cha mwezi mmoja, wakijaribu kupambana na changamoto zao na mwisho wa siku wanakuwa na maamuzi ya kutengana au kuendelea kuishi pamoja.
Siri ya mafanikio?
“Vipindi vingi vya namna hii huwa vimeandaliwa kimaandishi, ila sio cha kwetu, kwani chetu ni cha kihalisia zaidi,” anasema Kefa Hussein Igilo, mmoja ya watengeneza filamu ya Wa Milele?.
Hali kadhalika, kulingana na Igilo, ambaye pia ameshirikiana na Jerryson Onasaa katika kuandika na kuzalisha filamu ya Wa Milele?, filamu hiyo ilichaguliwa kushinda tuzo hiyo kutokana na ubora wa maandalizi mazima ya kazi hiyo, hasa katika upande wa ubora wa picha, ubora wa maudhui matumizi ya lugha ya Kiswahili, toka ilipoanza kurushwa hewani Novemba 22, 2024.
“Filamu yetu ni ya utofauti sana, ukilinganisha na zingine,” anajinasibu.
Mwanzo mgumu
Hata hivyo, haikuwa safari rahisi kwa mtengeneza filamu huyo, kung’ara kwenye tuzo hizo, kwani aliweza kushiriki kwenye AMVCA kupitia filamu ya ‘Love Transfusion’, mwaka jana, japo haikufanya vizuri.
Ila mwaka huu, wawili hao wamejihakikishia tuzo na kitita cha fedha, ambacho bado hakijawekwa wazi.
“Tunauona msimu wa pili wa Wa Milele? ukiwa wa kishindo…malengo yetu ni kuteka soko la Afrika Magharibi ambalo limeshikiliwa kwa muda mrefu na Nigeria na Afrika Kusini,” anaiambia TRT Afrika katika mahojiano maalumu.
Tasnia ilikosea wapi?
Kulingana na Kefa, kilichowaangusha watengeza filamu wengi nchini Tanzania, ni kushindwa kuzalisha filamu zenye ubora, hasa katika maudhui na picha.
Hata hivyo, anatoa ombi maalumu kwa wapenda filamu nchini Tanzania.
“Watanzania watuunge mkono kupitia kazi zetu, watu wapende kazi zenye maudhui ya Kiswahili, kwani kina uzito wake,” anaeleza.