Waziri wa Sheria wa Rwanda Emmanuel Ugirashebuja amemshukia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Maxime Prevot, kwa kushindwa kufuata kile anachokisema.
Akizungumza siku ya Jumanne, Ugirashebuja alidai kuwa kauli za Prevot zilikuwa tofauti na matendo yake.
Katika mahojiano yake na chombo cha habari cha Ubelgiji, Prevot alinukuliwa akisema kuwa nchi yake itaendelea kuheshimu misingi ya haki za kibinadamu.
Uhusiano kati ya Rwanda na Ubelgiji uko katika hali ya sintofahamu, hususani baada ya Rwanda kusitisha uhusiano wa kimaendeleo na Ubelgiji, na uamuzi wa Rwanda kuwafurusha wanadiplomasia wote kutoka Ubelgiji siku ya Jumatatu.
Machi 16, 2025, Rais Paul Kagame wa Rwanda aliionya Ubelgiji dhidi ya kuingilia maendeleo na mafanikio ya nchi yake, akiishutumu Ubelgiji kwa kuilaumu Rwanda kuhusika na machafuko yanayoendelea mashariki mwa DRC.