Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Sudan, Ibtissam Mohammed Ahmed, hakuwahi kufikiria kwamba siku moja angekimbilia katika shirika la misaada ili kupata chakula.
Huku mkataba wake muda wa Chuo Kikuu ukiwa umesitishwa kwa sababu ya vita vinavyoendelea hivyo kukosa fedha za kujikimu, Ahmed sasa anategemea jiko la jumuiya lililo karibu nae, maarufu takiya, kwa mlo wa kila siku katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
“Hali hii inatuathiri sana kisaikolojia, lakini unapokuwa huna mshahara, hakika itabidi uende takiya,” Ahmed alisema.
Mlima wa vyombo vya plastiki hupangwa katika majiko hayo ya jumuiya yanayoendeshwa na watu wa kujitolea, yanayojulikana kama "takaya" (wingi kwa takiya).
Huwakilisha mojawapo ya mila na tamaduni za kidini nchini Sudan ambazo zinalisha familia zilizo hatarini.
"Mwaka mmoja au miwili iliyopita, nililazimishwa kustaafu. Nilipewa mkataba na Chuo Kikuu, na kwa sababu taaluma yetu ni adimu na inafundishwa Chuo Kikuu, wanaboresha mikataba yetu kila mwaka - isipokuwa kwa mwaka huu wa vita, walituomba radhi wakisema hakutakuwa na kazi mpya kwa sababu hakuna rasilimali, na hata pesa walizokuwa nazo ziliibiwa," Ahmed anasema.
Huku mzozo nchini Sudan ukiingia katika mwaka wake wa pili, takaya zimekuwa nguzo muhimu katika kile maafisa wa juu wa misaada wanachosema "mgogoro mkubwa na mbaya zaidi wa kibinadamu duniani" katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita.
Vita hivyo, vita vilivyozuka Aprili 2023 huku kukiwa na mzozo wa kuwania madaraka kati ya Wanajeshi wa Sudan na Wanajeshi wa Rapid support Forces (RSF) kabla ya mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.
Huko Riyadh, Tareq Karrar akiwa na kaka yake pacha Karrar, macho yao yameelekezwa kwenye skrini ya simu wakifuatilia juhudu za kupata msaada kwa ajili ya kulisha watu.
Kilichoanza mwaka 2017 kama mpango wa kawaida wa kusambaza "mifuko ya Ramadhani" kimekuwa mojawapo ya juhudi za mashinani kusaidia familia za Sudan kama za Ibtissam wakati wa mgogoro.
Kwa mpango wa Tareq, ambao ulikua ukihudumia zaidi ya familia 700 kufikia 2023, mzozo ulilazimisha mabadiliko katika uendeshaji.
Baada ya kukimbilia Saudi Arabia na kaka yake, Karrar alieleza kuwa kutokuwepo kwao Sudan kumebadilisha mbinu zao.
Huku vita vimeathiri njia ya kufikia familia zenye uhitaji, wameelekeza mtazamo wao kwa kusaidia jamii kupitia mpango maarufu kama “ takaya.”
Ucheleweshaji wa mawasiliano ni changamoto kwani ujumbe unaotumwa kupitia WhatsApp huenda usipokee majibu kwa hadi siku tatu kutokana na kukosekana kwa mtandao wa uhakika.
Hali ya uchumi inazidi kutatiza juhudi zao, kwani bei ya vyakula hutofautiana kati ya mikoa. Usaidizi uleule wa kifedha ambao unaweza kuendeleza takiya kwa wiki mbili katika eneo moja unaweza kuisha kwa siku moja katika eneo jengine, hasa katika maeneo ambayo sio salama.
Huko Omdurman, sufuria kubwa za maharagwe zinachemka katika moja ya takaya ambayo hupokea usaidizi kutoka kwa mpango wa Tareq.
Mmoja wa waratibu ni Hanaa Gaafar, mfanyakazi wa kujitolea anayesimamia usambazaji wa misaada.
Juhudi zake zilianza miezi sita baada ya vita kuanza, awali alipika sufuria tatu kubwa za chakula kupitia michango.
Walakini, wakati Vikosi vya RSF vilipochukua mji wa Madani, operesheni yake ilibidi kupungua.
"Tunakusanya michango kwa kuwahimiza watu na kutuma picha na nyaraka kujaribu kuwafikia watu nje ya nchi na kutusaidia kukusanya pesa kwa ajili ya Takaya," Gaafar alielezea.
Katika nyumba ya jirani yake, wafanyakazi wa kujitolea wanafanya kazi pamoja kujaza vyombo na maharagwe huku Hanaa akitumia mitandao ya kijamii kama chombo muhimu cha kuchangisha pesa.