Ushawishi wa Qatar kuleta suluhisho kwenye mgogoro mashariki mwa DRC?
AFRIKA
4 dk kusoma
Ushawishi wa Qatar kuleta suluhisho kwenye mgogoro mashariki mwa DRC?Mnamo Machi 18, kiongozi wa Qatar, kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, aliwakutanisha Marais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa DRC jijini Doha, kwa nia ya kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wakutana na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani mjini Doha / Reuters
19 Machi 2025

Katika kikao na kiongozi wa Qatar, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, walitoa wito wa kusitishwa kwa machafuko katika eneo la mashariki mwa DRC.

Hii ni mara ya kwanza, kwa viongozi hao kukubaliana hivyo toka waasi wa M23 waongeze mashambulizi yao mwezi Januari 2025.

"Viongozi hao wameonesha utayari wao katika usitishwaji wa vita hivyo bila masharti yoyote kama ilivyokubaliwa jijini Dar es Salaam,” ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Qatar.

Hata hivyo, bado haijajulikana iwapo mazungumzo hayo yatazaa matunda.

"Wakuu hao wa nchi walikubaliana juu ya haja ya kuendelea na majadiliano yaliyoanzishwa huko Doha ili kuweka misingi imara wa amani ya kudumu kulingana na machakato wa Luanda/Nairobi, ambao sasa umeunganishwa,” ilisema taarifa hiyo.

Nini matokeo ya mazungumzo hayo?

Kwa sasa, nchi zote mbili hazijatoa maelezo ya kina kuhusu namna zitakavyositisha mapigano hayo.

Mazungumzo ya Doha, yanakuja siku moja baada kikundi cha M23 kususia mazungumzo ya amani ambayo yalipangwa kufanyika jijini Luanda nchini Angola, Machi 18, 2025, chini ya uratibu wa Rais João Lourenço wa Angola.

Hapo awali, kikundi hicho kilitoa wito wa kusitishwa kwa kile inachokiita mateso dhidi ya jamii ya Kitutsi nchini DRC.

Kinshasa imesema waasi hao ni magaidi na lazima waweke silaha chini.

"Kwa nini M23 wasimamishe vita ikiwa wanahisi wana nguvu kijeshi?" alisema Jason Stearns, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Simon Fraser, aliyebobea katika eneo la Maziwa Makuu.

"Unapochanganya hilo na vikwazo vilivyowekwa kwa Rwanda ambavyo vilikuwa vikali kuliko ilivyotarajiwa, nadhani waliona haukuwa wakati mwafaka kwao."

Rwanda imekana madai ya kuunga mkono kikundi cha M23 na kusema jeshi lake limekuwa likijilinda dhidi ya jeshi la DRC na wanamgambo wa FDLR wanaoishambulia Kigali.

Nini hatama ya juhudi za amani za kiafrika?

Kitendo cha Rais Kagame na Tshisekedi kukubali kukutana chini ya Qatar kinaibua maswali juu ya imani ya viongozi wa Afrika katika mikakati ya kikanda katika kutatua mzozo wao.

Kupitia ukurasa wake wa X, ikulu ya Kinshasa imesisitiza kuwa yale yaliyokubaliwa mjini Doha, yatawekwa wazi siku zijazo.

Mchakato wa amani wa Umoja wa Afrika unaongozwa na Angola, unajulikana kama ‘majadiliano ya Luanda’, wakati ule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulikuwa ukisimamiwa na Rasi wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Makubaliano hayo yalivunjika mwezi Disemba baada ya upande wa upinzani nchini DRC kufanya mazungumzo na DRC.

Mara kadhaa, wakuu wa Jumuiya za EAC na SADC wamejaribu kuwahimiza kumaliza tofauti zao, wakati wa mkutano wao uliofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 2025.

Tangu mwaka 2022, Umoja wa Afrika umekuwa ukimtumia Rais João Lourenço wa Angola, kufanya michakato ya upatanishi.

Hata hivyo, Rais Kagame na Tshisekedi wanaonekana kupuuzia jitihada mbalimbali barani Afrika, na kuwa tayari kukutana pamoja mbele ya kiongozi wa Qatar.

Suluhu ya DRC ni DRC yenyewe

Hii si mara ya kwanza kwa nchi ya DRC kujikuta katika matatizo kama haya.

Ni muhimu kufahamu kuwa, ni kupitia mazungumzo ya ndani, yaliyofanyika kati ya mwaka 2001 na 2003, DRC ilifanikiwa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mkataba wa kumaliza mapigano ya awamu ya pili nchini DRC, maarufu kama ‘Mkataba wa Sun City’ ulitiwa saini Aprili 2, katika hoteli ya Sun City, iliyoko Afrika Kusini.

Makubaliano hayo yalihusisha serikali DRC, chama cha RCD, MLC, mashirika ya kiraia na taasisi zingine.

Wakati huo Joseph Kabila alikuwa rais wa DRC.

“ Sidhani wapatanishi na wawezeshaji watafanya kitu kizuri zaidi kuliko tulivyofanya huko Suncity na ndiyo maana nikazungumzia kurejea kwenye mambo ya msingi kwa sababu makubalino hayo yalituwezesha kuwa na katiba miaka mitatu baadaye,” alisema Joseph Kabila, Rais wa zamani wa DRC katika mkutano wake na waandishi wa habari nchini Afrika Kusini.

Kiongozi huyo mstaafu, pia alikutana na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, Machi 18, 2025 kujadili hali ya usalama nchini DRC.

Kabila anasisitiza kuwa mzozo wa DRC unahitaji suluhu za kudumu za ndani na sio kuwatupia lawama wengine.

“ Mtazamo wangu kwa kila kitu kinachotokea unaweza kuulizwa katika swali moja: Ikiwa mimi ni mdhaifu ni kosa la nani? Je, ni kosa la jirani yangu au adui wangu au ni kosa langu?Ukijibu hili utapata suluhu,” alisema Rais Kabila.

“ Congo haiwezi kuendelea kuwa kama mtoto mchanga wa kulia lia, katika eneo hilo ikizungumzia jinsi ilivyo dhaifu na jinsi kila mtu ana nguvu. Hiyo kwangu sio njia sahihi.”

Kabila anasema DRC ina uwezo wa kujikwamua kwa kuhuhusisha wa Congo katika mjadala wa amani.

"Mwaka 2018 nilishiriki mkutano wa mwisho wa jumuiya ya SADC kama rais wa DRC na niliwaambia viongozi kuwa nafurahi kuondoka lakini Congo haikuwa tena nchi ya wanyonge katika eneo la maziwa makuu,” alieleza Kabila.

Kulingana na Rais Kabila, ni vyema DRC irudi kwenye msingi wa mzozo wa mashariki mwa nchi yake ambao anasema unahusisha makosa ya kutoheshimu sheria ya nchi.




CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us