Umoja wa mataifa unaonyesha hofu yake kwa kile ilichokiita “mashambulizi ya kiholela katika maeneo ya Sudan Kusini.”
Imesema Sudan Kusini inaelekea ukingoni mwa kurejea katika vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe huku ghasia zikiongezeka na mivutano ya kisiasa ikizidi.

TRT Global - Kutokuaminia kati ya Rais Salva Kiir na Naibu wake Riek Machar kunaibua hofu ya kimataifa kwamba taifa hilo changa zaidi barani Afrika, linarejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Mgogoro utafuta mafanikio yote yaliyopatikana kwa bidii tangu mkataba wa amani wa 2018 ulipotiwa saini. Utaharibu sio tu Sudan Kusini lakini eneo zima, ambalo haliwezi kumudu vita vyengine," Nicholas Haysom Mkuu wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini aliwaambia waandishi wa habari Machi 24, 2025.
Haysom alikuwa akiwahutubia waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kupitia kiungo cha video kutoka Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.
Amesema ni muhimu pande zinazozozana kuacha uhasama na kujitolea kuleta amani kabla ya nchi hiyo kutumbukia katika mzozo mwengine mbaya.
Wimbi la hivi punde la ghasia lilizuka tarehe Machi 4 wakati wanaojiita White Army - wanamgambo wa vijana - walipovamia kambi ya jeshi la Sudan Kusini huko Nasir, jimbo la Upper Nile.
Vikosi vya Serikali vilianzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya angani kwenye maeneo ya raia, kwa kutumia mabomu ya mapipa ambayo inadaiwa yalikuwa na viongeza kasi vinavyoweza kuwaka.
"Mashambulizi haya ya kiholela dhidi ya raia yanasababisha hasara kubwa na majeraha ya kutisha, hasa kuchomwa moto, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto," Haysom alisema, akiongeza kuwa angalau watu 63,000 wamekimbia eneo hilo.
UN inasema ripoti zinaonyesha kuwa Jeshi la White Army na vikosi vya kitaifa vinajipanga kwa makabiliano zaidi, huku kukiwa na madai ya kuajiri watoto katika vikundi vyenye silaha.
Kutumwa kwa vikosi vya kigeni kwa ombi la Serikali kumeongeza mvutano zaidi, na kuibua kumbukumbu za vita vya awali vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
“Mvutano wa kisiasa pia unaongezeka,” Haysom aliongezea.
Maafisa wakuu wanaohusishwa na Sudan People’s Liberation Movement in Opposition (SPLM-IO) - upande wa upinzani - wameondolewa, kubadilishwa, kuzuiliwa, au kulazimishwa kwenda mafichoni.
Pia kuna ongezeko la matumizi ya taarifa potofu na matamshi ya chuki, ambayo yanachochea migawanyiko ya kikabila na hofu, na kufanya maridhiano kuwa magumu zaidi.
"Kutokana na hali hii ya kutisha, hatuna jengine, lakini kutathmini kwamba Sudan Kusini inaelekea ukingoni mwa kurejea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe," Afisa huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa alionya.