AFRIKA
3 dk kusoma
Ethiopia kuwakata wafanyakazi mishahara kwa ajili ya mfuko wa dharura
Muswada ulio bungeni unalenga kuanzisha Tume ya Kudhibiti Hatari ya Maafa ya Ethiopia kama chombo huru cha serikali, chenye vifungu vinavyoamuru michango ya kifedha kutoka kwa sekta mbalimbali.
Ethiopia kuwakata wafanyakazi mishahara kwa ajili ya mfuko wa dharura
Ethiopia ilikumbwa na maporomoko ya ardhi 2024 katika Kusini mwa nchi iliyowauwa watu . Picha: Reuters / Reuters
20 Machi 2025

Muswada mpya uliowasilishwa kwa wabunge nchini Ethiopia unapendekeza kukatwa kwa mishahara kutoka kwa wafanyakazi wa serikali, na wa sekta binafsi na kuelekeza katika ufadhili wa misaada ya maafa.

Muswada huo unalenga kuanzisha Tume ya Kudhibiti Hatari ya Maafa ya Ethiopia kama chombo huru cha shirikisho, chenye vifungu vinavyoamuru michango ya kifedha kutoka kwa sekta mbalimbali.

Mfuko wa Kukabiliana na Hatari ya Maafa wa Ethiopia, kulingana na muswada huo, utatumika kwa "kupunguza hatari ya majanga, kukabiliana na juhudi za ukarabati" katika awamu tofauti za usimamizi wa hali hiyo.

"Fedha zilizokusanywa zitatumika wakati kutakapokuwa na pengo kwenye bajeti kwa ajili ya kukabiliana na hatari ya maafa yatakayotambulika kwa haraka kuziba pengo katika tukio la maafa ya ghafla," muswada huo unasema.

Sheria hiyo pia inahitaji michango kutoka kwa mabenki, taasisi ndogo za fedha, watoa huduma za benki kidijitali, na makampuni ya bima. Unasema fedha hizi zinaweza kukusanywa kupitia ada za huduma kama vile riba ya mikopo, ada za huduma za benki kidijitali, malipo ya awali na gawio.

Pendekezo lingine ni fedha zitozwe kwa huduma za pasipoti na viza, mauzo ya wasambazaji wa mafuta, na ada za leseni ya biashara.

Vyanzo vya ziada vya mapato ni pamoja na "mauzo ya tiketi za ndege, huduma za mawasiliano ya simu, wasambazaji wa mafuta, pasipoti na huduma za viza, na ada za leseni ya biashara."

Muswada unapendekeza kuwa mashirika ambayo yatashindwa kutii sheria yatakabiliwa na adhabu, ikiwa ni pamoja na malipo ya ziada ya 10%, na riba ya benki iliyoongezwa.

Serikali inajitayarisha kwa maafa

Kulingana na wizara ya fedha, Ethiopia imeathiriwa na ukame, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, mashambulizi ya wadudu, maporomoko ya ardhi, moto wa nyika, volkano, tetemeko la ardhi na migogoro.

“ Takriban watu milioni 2.2 na watu 175,000 wameathiriwa na ukame na mafuriko, mtawalia, kwa wastani kila mwaka katika miongo miwili iliyopita,” wizara ya fedha ya nchi hiyo imesema katika ripoti yake ya mkakati wa kufadhili hatari ya maafa 2023 hadi 2030.

Inasema uwezekano wa kuathiriwa na tatizo la maafa unazidishwa na kiwango cha juu cha umaskini nchini na utegemezi wake kwa sekta muhimu ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi: kilimo, maji, utalii na misitu.

“Ethiopia inakabiliwa na matukio kadhaa ya mabadiliko ya hali ya hewa na maafa. Ingawa usaidizi wa baada ya maafa kutoka kwa wafadhili unaleta unafuu muhimu, haisaidii sana kutokana na kiwango cha maafa kisichotabirika,” imeongeza.

“ Hii husababisha watu au mashirika machache kujitokeza, kuchelewa au kuwa kwa kiasi kidogo, na haichangii kulinda riziki au mafanikio ya maendeleo kwa ufanisi, wala haiendelezi ukuaji wa uchumi katika mazingira mazuri ya biashara.” ripoti hiyo iliongeza.

Muswada huo umepelekwa kwa Kamati ya Masuala ya mambo ya nje na amani kwa ukaguzi zaidi.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us