Simulizi ya mapambano ya kudai uhuru katika eneo la Afrika Magharibi haiwezi kukamilika bila kumtaja Samory Toure.
Baadhi ya waandishi wa vitabu wanamuona kama “mfalme shujaa”, kutokana na ushindi wake kwenye mapigano.
Wengi humuita shujaa kutokana na mchango mkubwa kwa watu wake.
Mwanzo wa shujaa
Ufanisi wa Toure kijeshi haukuwa kwenye kushinda vita tu, bali ngao yenye kulinda eneo la Afrika Magharibi.
Ushujaa wake uligusa vizazi vya Afrika Magharibi ili waweze kujiamini.
Toure aliishi kwa miaka 70, kati ya 1830 hadi 1900, na kuitengeneza historia ya Afrika Magharibi.
Mapambano dhidi ya ubepari
Kabla ya wakoloni kuchora mipaka yao barani Afrika, eneo la Afrika Magharibi lilishamiri kwa shughuli mbalimbali.
Hata hivyo, ilipofika miaka ya 1800, Ufaransa ikaanza kampeni ya kulitawala eneo la Afrika Magharibi.
Eneo hilo lilihusisha mataifa ya Senegal, Mali, Guinea, Benin, Burkina Faso, Mauritania, Niger na Ivory Coast.
Toure alipambana na Wafaransa wakati taifa hilo lilipoanza hatua za kutawala eneo la Afrika Magharibi.
Mfanyabiashara awa shujaa
Akiwa amezaliwa katika eneo la mashariki ya Guinea liitwalo Kankan, Toure alifuata nyayo za baba yake za kufanya biashara.
Pia aliamua kutumia elimu yake ya dini kama msingi wa kuendeleza biashara yake.
Hata hivyo, ilipofika mwaka 1853, ukoo wa Cisse ulimteka mama yake Toure wakati wa kutafuta watumwa.
Ili amuokoe mama yake, Toure alijitoa kama mtumwa kwenye ukoo wa Cisse.
Baada ya miaka saba ya kukaa utumwani, Toure alikuwa mtu huru, na huo ndio ukawa mwanzo wa kiongozi shupavu.
Aliporudi nyumbani mashariki mwa Guinea, alikusanya watu kutoka ukoo wa Camara, na kutengeneza jeshi imara.
Ushawishi
Toure aliwafundisha watu hao mbinu za kijeshi, akiongezea na elimu ya dini ya Kiislamu.
Ushawishi wa Toure ulizidi kukua hadi maeneo ya Mali, kaskazini mwa Guinea na Sierra Leone, Liberia na Ivory Coast, huku jeshi lake likizidi kuongezeka.
Hichi ni kipindi ambacho Wafaransa walikuwa wanaanza kusaka udhibiti wa eneo la Afrika Magharibi, huku jeshi la Toure likiwa na idadi ya vikosi 65,000.
Kutokana na ukubwa wa jeshi lake, Toure alifanikiwa kuingiza silaha kutoka nchi jirani ya Sierra Leone, ambayo ilikuwa chini ya utawala wa Waingereza.
Akiwa na jeshi kubwa nyuma yake, Toure alifanikiwa kudhibiti machimbo ya dhahabu karibu na mpaka wa Guinea na Sierra Leone.
Toure alikuwa na hamu ya kurejesha tena himaya ya Mali, iliyokuwepo kati ya miaka 1200 na 1600.
Toure alijua kuwa hatofanikiwa katika mkakati huu, na akaamua kutumia rasilimali kukuza elimu ya Kiislamu katika eneo la Afrika Magharibi.
'Napoleon wa Afrika'
Jitihada za Toure zilifanikisha ukuaji wa dini ya Kiislamu katika maeneo ya Guinea, Ivory Coast, Mali, Sierra Leone na Liberia katika karne ya 19.
Mnamo mwaka 1881, Wafaransa walijaribu kuiharibu himaya ya Toure, bila kufahamu kile kilichokuwa kikiwasubiri.
Jeshi la Toure lilipigana na Wafaransa na kuwashinda katika raundi ya kwanza, hatua iliyomfanya apewa jina la "Napoleon wa Afrika".
Wakiwa hawajaridhika na kichapo hicho, Wafaransa wakijapanga upya na kujaribu kupambana na Toure kwa mara ya pili, miaka miwili na ndipo mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ukafanyika.
Hatua hii ilimaanisha kuwa ushupavu wa Toure ukawa chini ya wakoloni.
Makubaliano
Ilipofika mwaka 1886, Toure aliingia makubaliano matatu na Wafaransa, ikiwemo kuachia eneo la Sierra Leone na Niger.
Mwaka 1891, Ufaransa ilivamia jeshi la Toure, hatua iliyomfanya kuachia maeneo muhimu ya Guinea, ambayo ni nchi yake ya asili.
Mji mkuu wa Conakry ukawa chini ya udhibiti wa Wafaransa.
Urithi wa Toure uliendelea nchini Guinea kupitia kitukuu chake Ahmed Sekou Toure, ambaye alikuwa na mchango kubwa katika upatikanaji wa uhuru wa nchi hiyo na kisha kuiongoza nchi hiyo hapo baadae.