Uchaguzi wa Alhamisi utafanyika katika mji wa kale wa Olympia. Na wagombea wote saba walipata nafasi ya kujumuika na wajumbe 109 watakaopiga kura ya siri eneo hilo.
“Ugiriki na ustaarabu wa Kigiriki umeipa dunia mambo mawili mazuri — demokrasia na michezo ya Olimpiki,” alisema rais wa IOC Thomas Bach, ambaye amefika ukomo wa miaka 12 inayoruhusiwa kukaa kwenye nafasi hiyo na ataondoka rasmi mwezi Juni.
Kuna wagombea watatu kati ya saba ambao huenda wakatoana jasho kwenye uchaguzi huo nao ni Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani Sebastian Coe, Waziri wa Michezo wa Zimbabwe Kirsty Coventry na Makamu wa Rais wa IOC Juan Antonio Samaranch.
Coe na Coventry wamewahi kuwa washindi wa Olimpiki — enzi zao kwenye riadha na uogeleaji, na Samaranch ndiye mgombea ambaye amekuwa mjumbe wa muda mrefu wa kamati ya IOC. Samaranch alijiunga na kamati hiyo 2001 wakati baba yake, ambaye pia anaitwa Juan Antonio Samaranch, alipoondoka uongozini baada ya kuwa rais kwa miaka 21.
Coventry huenda akawa mwanamke wa kwanza na raia wa kwanza kutoka bara la Afrika kuwa rais katika historia ya 131 ya IOC. Anaonekana kama mrithi ambaye Bach anamuunga mkono, jambo ambalo huenda likamhakikishia kura, ila hazitarajiwi kumpa ushindi katika hatua ya kwanza.
Wengine wanaogombea nafasi hiyo ni Mwanamfalme Feisal al Hussein wa Jordan, mjumbe wa kamati kuu ya IOC, na marais watatu wa mashirikisho mbalimbali ya michezo duniani:Johan Eliasch, ambaye ni bilionea; David Lappartient; na Morinari Watanabe wa Japan.
Mshindi wa uchaguzi wa Alhamisi lazima apate kura nyingi zaidi. Mgombea mwenye kura chache katika kila hatua ataondolewa kwenye uchaguzi. Rais wa Olimpiki anaongoza kwa kipindi cha miaka minane na anaruhusiwa kugombea tena kwa muhula mwingine mmoja wa miaka minne pekee.