Mohamed Salah ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya waandishi wa soka England kwa mara ya tatu baada ya kuisaidia Liverpool kushinda taji la 20 la EPL.
Salah amepata tuzo hiyo akiwa amefunga magoli 28 na kutoa ‘assists’ 18 kwa timu yake ya Liverpool msimu huu kwenye Ligi Kuu ya England.
Mshambuliaji huyo wa Misri amevunja rekodi ya EPL kwa kuhusika zaidi katika magoli kwenye mechi 38 za ligi hiyo huku Kocha Arne Slot akiwapa taji lao la kwanza tangu mwaka 2020.
Salah alipata kura za karibu asilimia 90 za waandishi wa mpira wa miguu England, ishara ya ushindi mkubwa zaidi karne hii.
Sawa na Thierry Henry
Beki wa Liverpool Virgil van Dijk alikuwa wa pili kwenye tuzo hizo, huku mshambuliaji wa Newcastle Alexander Isak akiwa wa tatu na kiungo wa Arsenal Declan Rice akichukua nafasi ya nne.
Salah, ambaye ameshinda tuzo hiyo msimu wa 2017-18 na 2021-22, sasa hivi yuko sawa kwa ushindi na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry kwa kuchaguliwa mara tatu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa 32 hivi majuzi aliondoa hofu kuhusu mustakabali wake baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili kubaki Anfield hadi 2027.
Uamuzi wa Salah wa kuendelea kubaki Liverpool kutawapa matumaini ya kushinda taji la 21 msimu ujao wakijaribu kuwashinda Manchester United kama klabu yenye mafanikio zaidi katika Ligi Kuu ya England.
Alessia Russo alikuwa mchezaji wa pili wa Arsenal kushinda tuzo hiyo upande wa wanawake,mshambuliaji huyo akimpiku mshindi wa mwaka jana Khadija Shaw.