Mwanadiplomasia huyu mkuu wa Uturuki amesema kuwa Ankara inafuatilia kwa ukaribu makubaliano kati ya Syria na SDF, yenye umiliki wa kikundi cha kigaidi cha PKK/YPG.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesisitiza haja ya kuwarudushia haki Wakurdi wa Syria, akiainisha misingi ya uraia, tamaduni, usawa wa kisiasa kama hatua muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya futari siku ya Jumatano, Fidan alielezea msimamo wa Uturuki kuhusu makubaliano kati ya Rais wa Syria Ahmed Alsharaa, na kikundi cha SDF, ambacho kinamilikiwa na YPG, ambalo ni tawi la Syria la kikundi cha kigaidi cha PKK, akisema kuwa Ankara inafuatilia kwa ukaribu maendeleo hayo.
“Tutafuatilia mchakato huo kwa utimamu,” alisema Fidan, akionesha hofu ya Uturuki kuhusu matokeo ya makubaliano hayo.
Wito wa kuiondoa Israeli nchini Syria
Fidan ameitaka Damasko kulipa kipaumbele suala la kuondoa vikosi vya Israeli ndani ya Syria, akisema kuwa serikali ya Syria iwe na udhibiti wa mchakato huo kwa uratibu wa jumuiya ya kimataifa.
Israeli imeendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Syria, yakilenga maeneo kadhaa.
Operesheni dhidi ya ugaidi yashika kasi
Kulingana na Fidan, nchi tano zimekutana mjini Jordan kuanzisha operesheni na intelijensia za pamoja dhidi ya kikundi cha kigaidi cha Daesh.
Alibainisha kuwa timu za ufundi zinaendelea kufanya kazi kuhusu mkakati huo, ikidhihirisha haja ya jitihada za kikanda za kupambana na ugaidi.
Ushirikiano kati ya Uturuki na Marekani na diplomasia kuhusu vita vya Ukraine
Akizungumzia uhusiano kati ya Uturuki na Marekani, Fidan alisema mazungumzo ya simu kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Marekani Donald Trump yalienda vizuri, akigusia heshima ya Trump kwa Erdogan.
Kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Fidan alisema kuwa Uturuki iko wazi kuchangia vikosi vya kulinda amani “iwapo pande hizo zitakubaliana kuanzisha” awamu moja ya mazungumzo siku zijazo.
Uturuki imekuwa na mchango mkubwa katika usuluhishi wa mgogoro kati ya Moscow na Kiev, ikiweza pia kufanikisha mradi wa ngano na ubadilishanaji wa wafungwa.
Jinsi mwenendo wa usalama wa kikanda unavyobadilika, ndivyo Ankara inavyozidi kujiweka kama kinara wa diplomasia, ulinzi, na vikosi vya usalama nchini Syria, Ukraine na eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla.