Watoto wa mitaani, wanavyotumia vipaji vyao kuleta furaha mjini Goma
Watoto wa mitaani, wanavyotumia vipaji vyao kuleta furaha mjini GomaWatoto waliopo katika kituo hicho, hutumia vipaji vyao vya kuimba na kucheza kutumbuiza na kuwachangamsha watu katika maeneo mbalimbali ikiwemo mitaani na hata katika soko maarufu mjini Goma.
Baadhi ya watoto wa kituo cha Invisible Kids kutoka Goma, DRC wakifanya mazoezi ya densi. Picha/ TRT World. / TRT Afrika Swahili
7 Mei 2025

Tangu 2017, Shule ya Invisible Kids imekuwa ikibadilisha maisha kupitia sanaa ya densi katika jiji la Goma nchini DRC.

Watoto waliopo katika kituo hicho, hutumia vipaji vyao vya kuimba na kucheza kutumbuiza na kuwachangamsha watu katika maeneo mbalimbali ikiwemo mitaani na hata katika soko maarufu mjini Goma.

Jeanne Kasilenge ambae anauza bidhaa katika soko hilo, anasimulia watoto hao wanavyoweza kuteka hadhira.

“Niliona jinsi watoto wanavyocheza, walicheza vizuri sana. Utendaji wao unathibitisha kwamba wanasimamiwa vizuri. Wana elimu nzuri, na wana adabu sana; inatia moyo sana kuona,” anasema Kasilenge.

Shule ya Invisible Kids ina zaidi ya watoto 20 na wanafundishwa ushirikiano na usafi.

“Tunapoamka, hatutaki kuona boma letu likiwa chafu, kwa hiyo tunajitahidi tuwezavyo kuweka safi kila kitu ndani ya nyumba na nje. Na hilo ndilo jambo tunalofanya na watoto wote. Lengo ni kuwafundisha kuwajibika wenyewe, ili waweze kufanya kazi zao wenyewe, hata kama sisi hatupo,” anasema Hassan Hakibab, ambae ni mwalimu shuleni hapo.

Densi ni njia ya watoto hawa ya kupumzika, na kusahau magumu ambayo wamepitia na kuangalia siku zijazo kwa jicho la matumaini.

Bush Sebar, ambae ni mwanzilishi wa kituo hiki, anasema kuwa, angependa kuchukua watoto wengi zaidi katika kituo chake, lakini uwezo wake haumruhusu.

“Hiki ni kituo cha watoto, tunaandamana na watoto ambao wengine ni yatima na wengine kutoka familia masikini. Ni kweli tunawafundisha densi, lakini pia wanapaswa kusoma, kuvaa na kuhudumiwa wanapokuwa wagonjwa. Hata hivyo, kutunza watoto ndio shauku yangu, na ningependa kuwatunza watoto wengine kwa njia yoyote niwezayo,” anasema Bush Sebar, mwanzilishi wa Invisible Kids.

Nae Zanem Nety Zaidi, ambae ni mwandishi ya makala hii, anasema kuwa kuna maelfu ya watoto wa mitaani Goma, wengi wao wakitoka katika familia zenye migogoro ambapo wanateseka mitaani kwa kukosa chakula na malazi bora.

Hata hivyo, baadhi ya watoto wanaoishi kituoni hapo, wanasema wamepata maisha mapya.

Munganga Esther, ambae ni Mkazi wa Invisible Kids anasema kuwa ana furaha kuishi na watoto wengine hasa kutokana na ushirikiano wao.

“Ushirika wa watoto wengine huniliwaza na kusahau kila kitu ambacho nimepitia maishani mwangu,” anasema Munganga Esther.

Kwenye majukwaa yao mbalimbali ya mitandao ya kijamii, video za densi za Shule ya Invisible Kids huvutia maelfu na kuibua hisia tofauti.

Pia wanatumbuiza katika hatua tofauti huko Goma, ambapo tayari wameshinda mashindano kadhaa ya kuimba na kucheza, hivyo kuwaletea umaarufu mkubwa.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us