AFRIKA
3 dk kusoma
Hatutaki vita na Eritrea, asema Waziri Kuu wa Ethiopia
Kumekuwa na hofu kuwa nchi hizo mbili huenda zinaamua kukunjiana ngumi kutokana na mvutano wa kisiasa baada ya kuvunja tena uhusiano mwaka 2022.
Hatutaki vita na Eritrea, asema Waziri Kuu wa Ethiopia
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed (kushoto) and Rais wa Eritrea Isaias Afwerki walitia saini makubaliano ya amani 2018 lakini mwaka 2022 uhusiano ukavunjika Graphics / TRT Afrika / TRT Afrika English
20 Machi 2025

Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema nchi yake haina nia ya kupigana na nchi jirani ya Eritrea.

"Ethiopia haina nia yoyote ya kujihusisha na mzozo na Eritrea kwa madhumuni ya kupata ufikiaji wa bahari,” Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliliambia Bunge siku ya Alhamisi.

“Nia yetu ni kushiriki katika mazungumzo na majadiliano juu ya suala hili,” ameongezea.

“Ufikiaji wa Bahari Nyekundu ni suala muhimu kwa Ethiopia. Tunachotaka ni kutatua kwa amani changamoto zetu za sasa."

Kumekuwa na hofu kuwa nchi hizo mbili huenda zikaamua kuingia vitani kwa sababu ya mvutano wa kisiasa.

Chanzo cha uhasama

Mahusiano yalichukua mkondo tofauti mwaka wa 2022 wakati serikali ya Abiy Ahmed ilipoamua kufanya makubaliano na chama cha Tigray People’s Front, TPLF.

Hiki ni chama kilichoko kaskazini mwa nchi ambacho wafuasi wake walipigana na serikali ya Abiy Ahmed kati ya 2020 na 2022. Ahmed aliwaona kama tishio la mapinduzi ya seriklai kwa kudai walishambulia kambi ya serikali yenye silaha.

Msingi wa TPLF, kaskazini mwa nchi ni mpaka wa Ethiopia na Eritrea.

Wakati wa vita hivyo, Eritrea ilimsaidia Waziri Mkuu Abiy Ahmed, lakini baada ya makubaliano ya 2022, Eritrea iliwachwa kando huku serikali ya Abiy Ahmed ikikaa meza moja na TPLF.

Wachambuzi wanasema Eritrea haikufurahishwa kwa kutengwa na makubaliano ambayo yaliruhusu TPLF, kuendelea na uongozi wake wa kaskazini mwa nchi.

Baadhi ya wanajeshi wa Eritrea wamesalia katika ardhi ya Ethiopia tangu kumalizika kwa mzozo huo, Marekani imesema, licha ya makubaliano hayo kutaka kuondolewa kwa vikosi vyote vya nje.

Kuvunjika kwa uhusiano

Eritrea, koloni la zamani la Italia lilitwaliwa na Ethiopia mwaka 1962.

Vikosi vya waasi wakiongozwa na Isaias Afwerki waliendesha mapambano ya miongo mitatu ya kivita ambayo yaliipatia Eritrea uhuru wake mwaka 1993.

Eritrea huru, ambayo bado inaongozwa na Isaias, awali ilifurahia uhusiano mzuri na Ethiopia, ambapo waasi wakiongozwa na viongoiz wa kabila la Tigray walimpindua mtawala wa kijeshi wa muda mrefu Mengistu Haile Mariam mwaka 1991 kwa msaada kutoka kwa waasi wa Isaias.

Lakini mapigano yalizuka mwaka wa 1998 kwenye mpaka kuhusu umiliki wa mji unaozozaniwa unaoitwa Badme, na kusababisha vita vya miaka miwili ambapo takriban watu 80,000 waliuawa.

Nchi hizo mbili zilisalia katika vita rasmi huku usafiri kati yao ukikatwa pamoja na huduma za mawasiliano .

Hata hivyo, baada ya miongo miwili haya yalibadilika baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuchukua uongozi 2018 na kuomba amani kutoka Eritrea.

Nchi hizo mbili zilikubali kurekebisha uhusiano wa kidiplomasia na kujenga upya uhusiano wa kiuchumi.

Lakini baada ya 2022, uhusiano wao umeanza kuzorota.

Matamko ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy tangu 2023 kwamba Ethiopia isiyo na bandari ina haki ya kutumia bahari imeongeza uhasama kati ya nchi hizo mbili.

Eritrea, ambayo iko kwenye Bahari Nyekundu, imeona matamko hayo kama tishio dhahiri la kuchukua hatua za kijeshi.

Septemba 2024, Shirika la Ndege la Ethiopia lilisitisha safari za ndege kwenda Eritrea baada ya akaunti yake ya benki kufungiwa.

Mwezi uliofuata, Eritrea ilitia saini mkataba wa usalama na Misri na Somalia ambao wataalamu wanasema haikuifurahisha Ethiopia kwani ina mvutano na Misri kwa sababu ya kukataa kuacha kujenga bwawa lake katika mto Nile licha ya Misri kusisitiza hivyo.

Pia Ethiopia na Somalia ziliingia katika mzozo wa kidiplomasia baada ya Ethiopia kufanya makubaliano na Somalialand ya kutumia sehemu ya bahari. Somalia imepinga hili ikidai kuwa Somaliland haina haki ya kufanya makubaliano ya aina yoyote kwani inaamini ni shemu ya Somalia.


CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us