AFRIKA
3 dk kusoma
Uganda yapeleka wanajeshi zaidi Sudan Kusini
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei Leuth, amesema kuwa uwepo wa jeshi la Uganda, UPDF chini ya Operesheni ‘Mlinzi wa Kimya’ ni nyongeza ya mpangilio wa muda mrefu wa usalama kati ya nchi hizo mbili.
Uganda yapeleka wanajeshi zaidi Sudan Kusini
Jeshi la Uganda linatuma wanajeshi zaidi nchini Sudan Kusini / photo: UPDF / Public domain
21 Machi 2025

Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi wa Uganda (UPDF), Luteni Jenerali Kayanja Muhanga, amewataka wanajeshi kuzingatia nidhamu na weledi wakati wakijiandaa kupelekwa Sudan Kusini chini ya "Operesheni Mlinzi wa Kimya."

“Kutumwa huko kunafuatia ombi la Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, akitaka uungwaji mkono wa haraka katika kuleta utulivu nchini humo baada ya mzozo kuzuka upya,” jeshi la UPDF limesema.

Jeshi la Uganda linaongea siku chache baada ya Serikali ya Sudan Kusini kukataa matamshi ya mkuu wa jeshi hilo Kainerugaba Muhoozi kuwa makomando wa UPDF walikuwa tayari nchini humo .

Kaimu afisa wa mawasiliano wa ulinzi, Chris Magezi amesema kanuni ya operesheni iliyopewa jina la ‘Operesheni Mlinzi wa Kimya’ ilizinduliwa Machi 11, 2025 kwa kuingizwa kwa vitengo maalumu vya operesheni.

“Viongozi kadhaa wa kikosi kazi cha UPDF tangu wakati huo wameimarisha misheni kupitia Bibia, Nimule kwenye mpaka wa kimataifa wa Uganda na Sudan Kusini,” Magezi amesema kupitia mtandao wa X.

Kamanda wa Kikosi Kazi cha Pamoja cha Hodari ni Brig. Jenerali Anthony Mbuusi Lukwago, kamanda mkongwe wa vita ambaye hadi hivi majuzi aliamuru wanajeshi wa Uganda wanaohudumu chini ya AUSSOM na Makao Makuu huko Mogadishu, Somalia.

Akitoa taarifa na kukiongoza kikosi hicho ambacho kiko chini ya uongozi wa Brigedia Jenerali Anthony Lukwago Mbuusi, Luteni Jenerali Muhanga aliwakumbusha wanajeshi hao dhamira yao kuu ya kudumisha amani na usalama nchini humo.

Wanajeshi wanaenda kufanya nini?

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei Leuth, alisema kuwa uwepo wa UPDF chini ya Operesheni ‘Mlinzi wa Kimya’ ni nyongeza ya mpangilio huo wa muda mrefu wa usalama.

"Serikali ya Sudan Kusini na serikali ya Uganda wana mkataba wa kijeshi ambao ulitiwa saini tangu wakati wa LRA," Makuei alisema.

"Mkataba huu haujabatilishwa, lakini tunautumia inapobidi. Vikosi vya UPDF vilivyofika Juba ni vitengo vya usaidizi na vitengo vya kiufundi. Vimekuja kusaidia kaka na dada zao katika jeshi la Sudan Kusini ,SSPDF," alisema.

Licha ya uhalali huo, wanaharakati wa upinzani wanahoji kuwa kutumwa kwa Uganda kunahusu zaidi kuimarisha serikali ya Rais Salva Kiir huku kukiwa na mvutano unaoongezeka na vikosi vya upinzani.

Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, hivi majuzi alitangaza kwamba hatua yoyote dhidi ya Kiir itachukuliwa kuwa "tangazo la vita dhidi ya Uganda."

Mgogoro nchini Sudan Kusini umeongezeka kufuatia mapigano mapya kati ya wanajeshi wa serikali na Jeshi la White Army, kikosi chenye nguvu cha wanamgambo wa Nuer ambacho kimehusika katika baadhi ya migogoro mibaya zaidi nchini humo.

Mapigano yameripotiwa katika Jimbo la Upper Nile, hasa karibu na Nasir, ambako helikopta ya Umoja wa Mataifa ilishambuliwa wiki iliyopita, na kusababisha kifo cha mfanyakazi na jenerali wa ngazi ya juu wa Sudan Kusini.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us