Kwa nini Kapteni Ibrahim Traoré anafananishwa na Thomas Sankara?
Kwa nini Kapteni Ibrahim Traoré anafananishwa na Thomas Sankara?
Mjadala huo umezuka kutokana na kufanana kwao katika umri, mtindo wa uongozi, msimamo wa kupinga ukoloni mamboleo, na taswira yao ya kizalendo.
13 Mei 2025

Kapteni Traoré alichukua uongozi wa Burkina Faso mwaka 2022 akiwa na umri wa miaka 34 tu, kupitia mapinduzi ya kijeshi, hali inayofanana kabisa na jinsi Sankara alivyoingia madarakani mwaka 1983 akiwa na miaka 33.

Wote wawili walijitokeza kama sauti ya wananchi waliokata tamaa, hususan vijana, wakiahidi ukombozi wa kweli na kujitegemea kwa taifa lao.

Traoré, kama alivyofanya Sankara, amekuwa mkosoaji mkubwa wa ushawishi wa mataifa ya Magharibi, hasa Ufaransa, katika siasa na usalama wa Burkina Faso na eneo la Sahel kwa ujumla.

Ameonesha msimamo wa kuondoa uingiliaji wa kigeni, kupinga utegemezi wa misaada, na kujenga mshikamano wa mataifa ya Afrika kwa sauti moja.

Anavaa mavazi ya kijeshi, anajieleza kwa ujasiri na unyenyekevu, na hujionyesha kama kiongozi wa watu.

Thomas Sankara alikuwa kiongozi wa mapinduzi na rais wa Burkina Faso kutoka mwaka 1983 hadi 1987.

Alijulikana kwa sera zake za kipekee za kujitegemea, upinzani mkali dhidi ya ukoloni mamboleo, na msimamo wake wa kuwapa wananchi uwezo wa kujikomboa kiuchumi na kijamii.

Alibadilisha jina la nchi kutoka Upper Volta kuwa Burkina Faso, “Nchi ya Watu Waadilifu”, na kuanzisha kampeni kubwa za uzalishaji wa chakula, chanjo kwa watoto, kupanda miti na kupigania usawa wa kijinsia.

Alikuwa kiongozi wa mfano kwa kutumia gari lenye gharama nafuu, kupunguza mishahara ya viongozi, na kuishi maisha ya kawaida pamoja na wananchi.

Sankara pia aliheshimika sana kwa kusimamia haki za wanawake, alipiga marufuku ndoa za kulazimishwa, alihimiza elimu kwa wasichana, na aliwateua wanawake katika nafasi za juu serikalini.

Licha ya mafanikio yake makubwa, aliuawa mwaka 1987 katika mapinduzi ya kijeshi yaliyopindua serikali yake, yaliyoongozwa na rafiki yake wa karibu Blaise Compaoré. Vile vile serikali ya Traore imeripoti kufelisha majaribio ya kupendua serikali yake.

Kwa hivyo, Traoré anapofananishwa na Sankara, si kwa sababu ya historia pekee, bali kwa sababu anaonekana kama anayefufua ari ile ile ya kizalendo, ujasiri wa kusimama na kusema hapana kwa uonevu wa kimataifa, na ndoto ya kuona Waafrika wakiandika hatima yao kwa mikono yao wenyewe.

Ingawa bado ni mapema kupima athari za uongozi wake, matumaini yameanza kuota upya miongoni mwa vijana wa Afrika, matumaini kwamba urithi wa Sankara haukufa, bali unazaliwa tena kupitia kizazi kipya cha viongozi jasiri kama Ibrahim Traoré.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us