Nchini Kenya kumekuwa na kampeni mtandaoni ambapo baadhi ya raia wa nchi hiyo, wanamtaka Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli ajiuzulu. Hii imetokea baada ya Atwoli kuwakashifu wanaharakati vijana maarufu Gen Z.
Lakini kwa nini kiongozi huyo wa wafanyakazi ajipate matatani?
Atwoli, amekuwa kiongozi wa muungano wa wafanyakazi tangu 2001, huku akitangazwa mshindi wa uchaguzi kila mara unapofanyika. Katika nyadhifa mbali mbali kiongozi huyo mwenye miaka 75 ametumikia chini ya marais wote wa Kenya tangu baba wa taifa la nchi hiyo Jomo Kenyatta, akifuatiwa na Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na sasa William Ruto.
Hivi majuzi alisema labda serikali ya Ruto itakuwa ya mwisho halafu astaafu, lakini mwezi Aprili, Bodi ya COTU ilimpitisha tena kama mgombea wa nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika 2026.
Iwapo atashinda katika uchaguzi huo, basi atashikilia nafasi hiyo kwa miaka mitano mengine. Hata hivyo, Atwoli, uongozi wake umevuka mipaka ya Kenya.
Yupo pia katika ramani ya kimataifa ambapo hivi sasa, yeye ni rais wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OATUU) na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Duniani.
Wakenya wanamjua Atwoli kwa maisha yake ya kifahari na kauli na vitendo vyake vya kujionyesha. Kwa mfano, 2019 aliibua gumzo mitandaoni alipotupa simu yake aina ya iPhone 11 pro max akiwa katika mahojiano studio.
Simu hiyo ambayo wakati huo ilikuwa ni toleo mpya ilikuwa na thamani ya zaidi ya dola 1,300 wakati huo.
Mwaka 2016, Atwoli alisema kuwa mavazi yake ya kila siku yana thamani ya takriban dola 10,000 ambazo zilikuwa ni sawa na shilingi milioni moja ya Kenya kwa wakati huo.
Aliendelea kudai pia, kwamba saa anayovaa ni miongoni mwa za bei ghali zaidi duniani, kama Franck Muller ambayo bei yake huanzia dola 2,400.
Pia anajigamba kumiliki majumba kadhaa ya kifahari nchini Kenya.Kauli za kiongozi huyu mkongwe wa wafanyakazi, siku zote zimekuwa zikiibua gumzo katika siasa za Kenya.
Kwa mfano mwaka wa 2020, alipendekeza katiba ibadilishwe ili kuwezesha Rais Uhuru kenyatta aongezewe majukumu baada ya kumaliza muhula wake 2022 akidai Kenyatta alikuwa bado ana umri mdogo.
Mwaka 2022, Atwoli alimfanyia kampeni ya wazi ya urais aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Raila Odinga akitoa kauli za kejeli kwa wakaazi wa Sugoi, ambapo Ruto anatoka kukata miti karibu na makazi ya Ruto kwa sababu anaweza kujiua baada ya kushindwa na Raila Odinga.
Baadaye Ruto akawa Rais na Atwoli akaonekana kumeza kauli yake ya kejeli na kuanza kunyenyekea.
Na Machi mwaka huu kiongozi huyo huyo mwenye umri wa miaka 75, alikuwa gumzo la alipotangaza kupata mtoto na mke wake wa pili.
Na huku akiendelea kupigwa vita mitandaoni, baadhi ya Wakenya hivi sasa, wameanzisha kampeni ya kutaka ajiuzulu, nae kwa kujitetea, amewaambia Wakenya, watamkumbuka, iwapo ataamua kujitoa katika wadhifa huo.