Jeshi la Sudan latangaza kuchukua tena Ikulu ya Rais huko Khartoum, ikulu hiyo ni ngome ya mwisho iliokuwa ikidhibitiwa na kikosi cha RSF kinachoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo.
Aidha, video na picha zimesambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha wanajeshi wa Sudan wakiwa ndani ya Ikulu kama ishara ya udhibiti huo.
Vita ndani ya jiji la Khartoum vimekua vikiendelea kwa kasi baada ya jeshi kuweza kuchukua udhibiti wa jimbo la Aljazeera na miji iliyokuwa karibu na Khartoum.
Uhasama kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya kikosi cha RSF umeanza mwezi Aprili 2023, na kusababisha mgogoro mkubwa Sudan, huku watu wengi wakilazimshwa kuyahama makazi yao.
Hata hivyo RSF, ambayo mapema mwaka huu iliunda serikali mbadala katika kongamano lililofanyika jijini Nairobi, inaendelea kushikilia udhibiti wa baadhi ya maeneo huko Darfur.
Jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa inaendela kutoa wito wa kusitishwa kwa vita, ikionya juu ya hali mbaya kwa raia huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula.