Ni mshambuliaji na sasa hivi yuko katika klabu ya Ligi Kuu ya Ugiriki ambayo ligi hiyo inajulikana kama Super League.
Timu anayocheza Samatta inafahamika kwa kifupi kama PAOK, kirefu chake ni ‘’Pan-Thessalonian Athletic Club of Constantinopolitans’’
Ni mzaliwa wa Dar es Salaam, Tanzania na ana umri wa miaka 32.Mbwana Ally Samatta maarufu ‘Captain Diego’ ameweka historia mpaka sasa, Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi Kuu ya England na pia ni raia wa kwanza wa Tanzania kufunga bao katika ligi hiyo.
Aston Villa
Alijiunga na Aston Villa akitokea Genk ya Ubelgiji Januari 2020 na mwezi uliofuata 1 Februari katika mechi yake ya kwanza akiwa kwenye uzi wa Villa kwenye Ligi kuu ya England akafunga goli dhidi ya Bournemouth. Lakini Aston Villa walipoteza mechi hiyo 2-1.
Amekuwa mchezaji wa Simba SC ya Dar es Salaam nchini Tanzania na pia TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mwaka 2015 alikuwa mchezaji bora anayesakata soka barani Afrika.
KRC Genk
Ni wazi kuwa ukali wa Captain Diego ulibainika alipokuwa na Ligi Kuu ya Ubelgiji akiwa na timu ya Genk kuanzia mwaka 2016 na kuisaidia klabu hiyo kuchukua ubingwa 2019. Pia alikuwa mfungaji bora wa ligi msimu huo.
Kwa ujumla alifunga mabao 56 akiwa Genk katika mechi 144 alizocheza.
Amekuwa mchezaji muhimu pia kwa timu ya nchi yake, Taifa Stars akiifungia magoli 22 katika mechi 83 alizocheza.
Mbali na Tanzania, Mbwana Ally Samatta amecheza soka katika mataifa ya DRC, Ubelgiji, Uingereza, Uturuki na Ugiriki, mechi nyingi zaidi zikiwa katika ligi za Ulaya.
Na huyo ndiye Captain Diego wa Tanzania.