Tanzania inawania nafasi nyeti ndani ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kanda ya Afrika, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule wa shirika hilo kwa kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile aliyefariki dunia Novemba 27, 2024.
Kwa sasa, Profesa Mohamed Yakubu Janabi ndiye anayepigiwa chapuo kumrithi Dkt Ndugulile, hasa baada ya WHO kupitisha jina lake, tayari kabisa kwa uchaguzi utakaofanyika Mei 18, 2025.
Profesa Janabi si jina geni ndani ya kuta za afya nchini Tanzania. Akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Tiba, Janabi amejizoelea umaarufu kutokana na ushauri wake wa kiafya, hususani mpangilio wa milo, ambao umewaacha baadhi ya watu vinywa wazi.
‘‘Taasisi zetu ambazo baadhi mimi nazisimamia, zimekuwa zikitoa huduma katika nchi mbalimbali zikiwemo Zambia, Malawi, Burundi na hata visiwa vya Comoro,’’ anasema Profesa Janabi. ‘‘Mimi pia nimeshiriki kusaidia wagonjwa hao, kwa mfano pale Rwanda, kwenye hospitali ya King Feisal, ambapo nilikaa kwa siku 10 nikifanya upusaiji.’’
Haya ni baadhi tu ya mambo mengi yaliyofanywa na gwiji huyo wa afya kwa zaidi ya miongo minne, akishiriki mafunzo mbali mbali, tafiti na hata kuandika machapisho zaidi ya 100 kwenye mada mbali mbali.
Anusurika kifo kwa Malaria
Mapenzi ya Profesa Janabi kwenye afya ya umma yalianzia tangu akiwa mtoto mdogo. Wakati fulani, Janabi aliwahi kuugua ugonjwa wa Malaria ambao ulitaka kugharimu uhai wake, na hapo ndipo hamu ya kujitolea kupambana na magonjwa ikamuingia.
‘‘Afrika ni bara la ustahimilivu, utofauti, na fursa. Ni eneo ambalo limekabaliwa na changamoto kubwa za kiafya,’’ anaongeza Profesa Janabi.
Miongoni mwa mambo muhimu anayotaja katika ilani yake, ni hamu yakuona mipaka ya afya ikifunguliwa, ili nchi zishirikiane zaidi katika kudhibiti magonjwa yenye kuambukiza.
‘‘Wanapozungumzia kuongeza uwezo kwa nchi jirani, sisi tumefanya kwa vitendo. kwa hiyo naamini nikiboresha zaidi hiyo njia, kuna siku Afrika itakuwa ikiagizia dawa kutoka Zimbabwe, Rwanda au Ethiopia,’’ anaambia TRT Afrika.
Uelewa wa magonjwa ya kuambukiza
Profesa Janabi pia ameshiriki udhibiti wa magonjwa mbalimbali kama vile Marburg kwa mwaka 2023 na 2025.
Michango yake katika utafiti wa kimatibabu ni pamoja na uchunguzi wa pamoja majaribio muhimu ya chanjo ya VVU (HIVIS, TaMoVac). Kwa sasa, Profesa Janabi ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya na Tiba.
Wakati wa mlipuko wa Ebola, uliodumu kati ya mwaka 2014 hadi 2016, Profesa Janabi alichukua jukumu muhimu katika kushughulikia janga hilo - nyumbani, na pia katika nyadhifa yake kama Mshauri Mkuu wa Sera ya Afya na Lishe wa Rais wa zamani wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Zaidi ya hayo, pia ameshirikiana na taasisi ya Bill Gates, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) na WHO kuimarisha Miundombinu ya afya ya Tanzania. Michango yake ilitambuliwa wakati Tanzania ilipopokea tuzo ya ‘Goal Keepers Award’ kutoka Gates Foundation, tuzo ya uvumbuzi wa huduma ya afya, kwa juhudi za nchi kupanua huduma za afya vijijini, kuboresha vituo vya matibabu, na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya ya jamii 137,000 kufikia mwaka 2030.
Anavaa viatu vya Ndugulile.
Profesa Janabi anawania nafasi hiyo kufuatia kifo cha ghafla cha Daktari Faustin Ndugulile, aliyefariki miezi michache kabla ya kushika wadhifa huo ndani ya WHO Afrika.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alionesha imani yake kwa Profesa Janabi, sio kwa uteuzi tu, bali kwa kumsindikiza na maneno ya kumtia moyo.
‘‘Najua katika kumrithi Dkt. Ndugulile, Profesa Janabi atatoa pongezi kwa kumbukumbu yake kwa njia bora ambayo anaweza - kupitia vitendo, huduma, na kujitolea,’’ alisema Rais Samia.
‘‘Mimi naamini kuwa chini ya uongozi wangu, tutafanya mabadiliko ndani ya WHO Afrika na kuhakikisha kwamba huduma ya afya sio fursa ya upendeleo, bali ni haki ya msingi kwa wote.’’
‘‘Afya na amani ndio chanjo bora zaidi kwa maisha.’’