Uso wa Marie Kanyere unaonesha ishara ya mama aliyekata tamaa wakati mtoto wake mdogo kati ya watoto wake wanne, akiwa na homa na kudhoofika, anatetemeka akiwa kwenye hema lao ambalo limejaa maji.
Anajuwa dalili hizi – huenda ikawa anaugua malaria. Hali inazidi kuwa mbaya alipofahamu kuwa hakuna dawa kwenye zahanati.
"Nilikimbia kutoka kwenye kijiji chetu wakati wapiganaji walipokuja. Walimuua kaka yangu na kuchoma nyumba yetu," Marie ameiambia TRT Afrika. "Hapa, tunalala kwenye matope, watoto ni wagonjwa, na hakuna chakula.Sijui kama ningekaa huko na kuuawa kama ingekuwa wazo bora kuliko kuja hapa kuteseka kila siku.”
Kambi ya wakimbizi ya Musenyi mashariki mwa Burundi, ambayo imepangiwa kuwa kambi ya muda, imekuwa sehemu iliyolemewa.
Ni safari ya saa tano kwa gari, kutoka katika mpaka wa Burundi na DRC ambapo kuna vita, ina watu zaidi ya ilivyotakiwa, inafurika kila inaponyesha mvua, na hakuna misaada inayofika huko.
Marie ni mmoja ya wakimbizi wa Congo 71,000 waliokimbilia Burundi tangu Januari, wakikimbia mapigano yaliyokithiri mashariki mwa DRC.
Misaada haitoshi kutokana na kukosekana kwa wafadhili duniani, na kuna wakimbizi wengine wapya wanaofika katika kambi hiyo.
Chanzo cha mgogoro
Mapigano haya mashariki mwa DRC yamechochewa na ugomvi kati ya makundi yenye silaha ili kudhibiti utajiri wa madini katika kanda hiyo.
Makundi ya wapiganaji zaidi ya 130 yako katika eneo hilo, ikiwemo kundi la M23, ambalo limechukua maeneo mengi katika miezi ya hivi karibuni likidaiwa kuungwa mkono na Rwanda. Rwanda inakanusha madai hayo.
"Mapigano haya ni vita kwa niaba ya watu wengine, watu wanaogombania madaraka na mataifa ya nje yanayotaka kunyonya utajiri wa eneo hilo," ameeleza Emmanuel Masamba, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini DRC.
"Raia wanajikuta katikati ya wapiganaji, vikosi vya serikali na maslahi ya mataifa ya nje, huku dunia ikiwa haishughuliki."
Serikali ya DRC, inayoungwa mkono na vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani na wanajeshi wa kanda,wamekuwa na wakati mgumu kuleta hali ya utulivu katika eneo hilo. Mauaji ya kikatili, dhulma za kingono na kuwaondoa watu kwa lazima kutoka katika makazi yao imekuwa jambo la kawaida.
Mzozo juu ya mzozo
Kambi ya wakimbizi ya Musenyi, sasa hivi ina watu 16,000, na haikujengwa ihifadhi idadi kubwa ya watu kiasi hicho.
Kuongezeka kwa mahema ya dharura katika maeneo yenye maji mengi, ambayo ardhi hiyo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya ukulima, kunadhihirisha tatizo kubwa. Na wakati wa msimu wa mvua, maji yaliyotuwama yanasababisha mlipuko wa maradhi, na mahema ya muda huwa yanaanguka kutokana na mvua kubwa.
" Huwa tunaona kuongezeka kwa ugonjwa wa malaria, kipindupindu na matatizo ya kupumua," anasema Dkt. Jean-Christophe Niyonzima, daktari anayefanya kazi na shirika moja lisilokuwa la kiserikali linaloshughulika na mambo ya afya.
"Watu ni wengi wanaotaka matibabu kwenye zahanati na hakuna dawa, wanawake wajawazito wanajifungua kwenye mahema yaliyojaa maji. Bila kupata usaidizi zaidi, watu watakufa kutokana na ugonjwa ambao unaweza kukingwa."
Hakuna shule, hamna vyoo visafi, na kuna uhasama kati ya wakimbizi na jamii ya eneo hilo wakigombana kuhusu raslimali chache zilizopo.
Hakuna hiari
Mazingira mabaya ya kuishi na kutokuwepo kwa misaada kumesababisha baadhi ya wakimbizi kurejea katika maeneo ya vita.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR linasema kuwa baadhi ya familia tayari zimevuka na kurejea DRC, wakijiweka katika hatari ya mapigano na kuungana tena na familia zao au kuokoa chochote kilichobaki katika nyumba zao.
"Mume wangu alirejea DRC wiki iliopita kuangalia kama ardhi yetu bado ipo," Sifa Ntamwenge, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 27, ameiambia TRT Afrika. "Nilimwambia asiende, lakini tutafanya nini? Hapa, tunakula mlo mmoja kwa siku kama tuna bahati."
Hata wakati baadhi ya wakimbizi wakiondoka katika kambi ya Musenyi, mamia zaidi wanaingia kila wiki, wakiwa wameondolewa katika makazi yao.
Kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha UNHCR na washirika wake wamepunguza utoaji wa huduma muhimu.
Hamna vifurushi vya heshima kwa wanawake na wasichana – ikiwa ni pamoja na sabuni, pedi na nguo za ndani – havitolewi tena, na kuwaacha watu 11,000 bila vitu muhimu vya usafi.
Miradi ya kuwaunganisha watoto waliotengana na familia zao imepunguwa, na hakuna maeneo salama kwa wanawake na watoto.
"Tulikuwa na kituo cha wanawake ambapo wale waliobakwa walikuwa wanapewa ushauri nasaha na matibabu," anasema Florence Niyonkuru, ambaye amefanya kazi na waathiriwa wa dhulma za majumbani nchini Burundi. "Sasa wanakuja kwetu, lakini hatuna cha kuwapa. Wengi wanaumia tu kimya kimya."
Taarifa za wanawake wanaokimbia kubakwa zinaongezeka nchini DRC, huku zaidi ya 60% wakieleza hayo kwa wafanyakazi wa kutoa misaada.
Mzigo kwa Burundi
Serikali ya Burundi imeonesha kile UNHCR inakiita "uongozi wa kupigiwa mfano” kwa kuwapa Wacongo walioondoka katika makazi yao hadhi ya ukimbizi pamoja na kuwapa ardhi. Lakini uwezo wa nchi hiyo unaishiwa nguvu kutokana na mapigano katika kanda, mfumuko wa bei na matatizo ya kiuchumi.
"Jamii zilizopo katika maeneo hayo zinatumia pamoja na wakimbizi kile kidogo walichonacho, lakini subira yao inapungua," anasema Pierre Ndayishimiye, afisa mmoja katika Mkoa wa Cankuzo. "Kama dunia haitosaidia, tatizo hili litaendelea kwa mataifa mengine."
UNHCR imetoa wito wa kupatikana kwa dola milioni 76.5 million ili kukabiliana na hali hiyo ya dharura nchini Burundi kama sehemu ya mpango mpana wa kusaidia wakimbizi wa Congo walioko katika mataifa saba ya barani Afrika. Bila fedha hizo, wataalamu wanaonya kuwa kutakuwa na janga baya zaidi.
"Tuko kwenye hali ya dharura, kuchagua nani apate msaada na nani asipate," anasema mtu mmoja anayejitolea na shirika la UNHCR nchini Burundi. "Hii siyo kazi ya kutoa misaada pekee; ni kufikiria kuhusu mbinu gani itatumika kuzuia janga kubwa zaidi."