Mchakato wa kumchagua papa mpya wa Kansia Katoliki umeanza rasmi katika Kanisa ya Sistine huko Vatican.
Makadinali 133 wameingia katika eneo hilo ambapo watakaa mpaka atakapopatikana kiongozi mpya.Tanzania, Sudan Kusini, Rwanda, Ethiopia, Jamhuri ya kidemokrais ya Congo, DRC ni kati ya nchi ambazo makadinali wake watashiriki kupiga kura. Vatican tayari imetoa tangazo kuwa minara ya simu itazimwa kuanzia Mei 7, 2025, hadi jina la papa mpya litakapotangazwa.
Ni hatua moja wapo ya kuzuia mawasiliano kati ya makadinali na ulimwengu wa nje.
Shauku kubwa iliyopo miongoni mwa waumini wa Kanisa Katoliki ni kutaka kujua, je, bara gani litaibuka kidedea katika kutoa papa mpya?
Kati ya makadinali 133 wanaopiga kura, 17 kati yao wanatoka Afrika.Ili Afrika itoe papa, inahitaji kupata theluthi mbili ya kura za jumla kama inavyohitajika. Hii ina maana, makadinali wa Afrika wote, itabidi wampigie kura mmoja wao bila kuzigawa.
Baada ya hapo mgombea wa Afrika atategemea kupata wastani wa kura 72 kutoka kwa makadinali wengine. Makadinali kutoka Ghana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni kati ya wale wanaotajwa na vyombo vya habari kuwa na uwezekanao wa kuchukua uongozi huo.
Hata hivyo, kutajwa tu sio tiketi ya ushindi.Katika historia ya Kanisa, kwa mfano, kuanzia miaka ya 1900, mapapa wengi walitokea Italia.Mtindo huu ulibadilika 1978 baada ya papa mwenye asili ya Poland alipopata kiti, baadae kufuatiwa na Mjerumani na na hatimae Papa Francis ambaye alikuwa raia wa Argentina.
Matumaini ya Afrika ya kuweza kuongoza Kanisa hilo yalikuja pale Papa Francis kutoka Argentina alipochaguliwa, kwa sababu nchi yake inaangaliwa kama nchi za Afrika zinazoendelea.
Kwa kwa sababu usiri wa kura hiyo, dunia haitajua ni nani aliyempigia nani kura, bali dunia itakachoshuhudia ni moshi tu mweupe, ukiashirika kuchaguliwa kwa Papa mpya.