India na Pakistan zimeshambuliana kwa makombora na mizinga katika hali ya kuongezeka kwa uhasama kati ya majirani hawa wenye silaha za nyuklia baada ya shambulio katika eneo linalozozaniwa la Kashmir.
Haya ndiyo tunayojua kuhusu mgogoro huu na historia yake.
Ni zipi habari mpya?
India ilianzisha kile ilichokiita "mashambulizi mahsusi yaliyolenga kambi za magaidi" katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na Pakistan mapema Jumatano.
Pakistan inasema raia 26 waliuawa katika mashambulizi hayo kwenye maeneo yasiyopungua sita pamoja na mapigano ya risasi mpakani.
Walilenga mahsusi maeneo ya Kashmir inayosimamiwa na Pakistan pamoja na miji ya Bahawalpur na Muridke, katika jimbo lenye idadi kubwa ya watu la Punjab, mpakani mwa India.
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Muhammad Asif, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa hatua ya kulipiza kisasi "tayari imeanza", baada ya jeshi kusema awali kuwa litalipiza "kwa wakati ambao wanaona kuwa sahihi."
India iliilaumu Pakistan kwa kushambulia kwa mizinga kuvuka Mstari wa Udhibiti (LoC), mpaka rasmi katika Kashmir, na kuua raia watatu.
Ndege za kivita za India zimedunguliwa
Msemaji wa jeshi, Ahmed Sharif Chaudhry, katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Islamabad alisema Pakistan imeangusha ndege tano za kivita za India zilizovuka mpaka, ikiwemo ndege tatu za kivita za Kifaransa aina ya Rafale, baada ya kuishambulia Pakistan.
Aliongeza kuwa kituo cha kufua umeme cha maji katika Kashmir inayosimamiwa na Pakistan pia kililengwa, na kusababisha uharibifu wa bwawa.
Afisa mkuu wa usalama wa India, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema ndege tatu za kivita za India zilianguka katika eneo la nchi yao. Mabaki ya moja ya ndege hizo yalionekana na mpiga picha wa AFP huko Wuyan, upande wa Kashmir unaosimamiwa na India.
Nini kilisababisha mgogoro huu?
India ilikasirishwa na shambulio la Aprili 22 lililofanywa na wapiganaji dhidi ya watalii katika Kashmir inayosimamiwa na India, ambalo liliua watu 26, wakiwemo Waislamu, katika eneo maarufu la utalii la Pahalgam.
Hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo lakini India ilisema washambuliaji walikuwa kutoka kundi la wapiganaji la Lashkar-e-Taiba lenye makao yake Pakistan, ambalo limeorodheshwa na Umoja wa Mataifa kama shirika la kigaidi lenye historia ya kufanya mashambulizi kwenye ardhi ya India.
Kundi hilo kwa muda mrefu limekuwa likihusishwa na jeshi la Pakistan, madai ambayo Pakistan inakanusha.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alilaumu Pakistan kwa kuunga mkono "ugaidi wa kuvuka mipaka" na akalipa jeshi lake "uhuru kamili wa kiutendaji" kujibu mashambulizi hayo.
Pande zote mbili ziliwafukuza wanadiplomasia, na wiki iliyopita Pakistan ilisema ilikuwa na "taarifa za kuaminika" kwamba India ilikuwa inajiandaa kwa shambulio la kijeshi.
Dunia imejibu vipi?
India na Pakistan zote zina silaha kubwa za nyuklia, na Kashmir kwa muda mrefu imekuwa ikitambuliwa kama moja ya maeneo hatari zaidi duniani kwa uwezekano wa vita vya nyuklia.
Kwa sababu hiyo, kumekuwa na wito wa kuwepo kwa utulivu kutoka kote duniani tangu mgogoro huu ulipoanza na shambulio la Aprili 22.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitoa wito wa "uvumilivu wa hali ya juu," msemaji wake Stephane Dujarric alisema katika taarifa.
"Mgogoro wa kijeshi kati ya India na Pakistan siyo mzuri kwa dunia," Dujarric alisema.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amezungumza na wenzake kutoka India na Pakistan, na kuwataka wote wawili wafanye mazungumzo.
China, jirani wa nchi zote mbili, ilielezea "masikitiko juu ya hatua ya kijeshi ya India asubuhi ya leo" na kusema ilikuwa "na wasiwasi kuhusu maendeleo ya sasa," katika taarifa kutoka kwa msemaji wa wizara ya mambo ya nje.
Urusi ilionesha wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa mgogoro kati ya India na Pakistan huku ikisisitiza kwamba "inakemea vikali vitendo vya kigaidi, inapinga aina zote za kuwepo kwake, na inasisitiza haja ya juhudi za pamoja za Jumuiya ya kimataifa kukabiliana na uovu huu."
Ufaransa ilitoa wito kwa India na Pakistan kuepuka kuongezeka kwa mgogoro na kulinda raia. "Tunaelewa lengo la India la kujilinda dhidi ya tatizo la ugaidi. Lakini tunatoa wito kwa India na Pakistan kuwa wastahmilivu, kuepuka kuongezeka kwa mgogoro na, bila shaka, kulinda raia," Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, alisema kupitia shirika la habri la Kifaransa la TF1.
Nani anadhibiti Kashmir?
Eneo la milima la Himalaya lenye mandhari nzuri limekuwa chanzo kikuu cha mzozo kati ya India na Pakistan tangu nchi hizo mbili zilipoasisiwa baada ya ukoloni wa Uingereza kumalizika mwaka 1947.
Mtawala wa Kashmir alisitasita kuamua kujiunga na India yenye idadi kubwa ya Wahindu au Pakistan yenye idadi kubwa ya Waislamu, hali iliyosababisha vita vya kwanza kati ya majirani hawa wawili.
Vita vingine vikubwa kati ya India na Pakistan juu ya Kashmir vilifuatia mwaka 1965 na 1999, huku kukiwa na uasi wa mara kwa mara na mapigano ya mpakani katika miaka kati ya hapo na baada ya hapo.
Pande zote mbili zinadhibiti sehemu ya Kashmir lakini zinadai eneo hilo lote, na kuweka wanajeshi waangalizi kwenye Mstari wa Udhibiti.
Pande hizo mbili zilikaribia vita vingine mwaka 2019 baada ya vikosi vya India 41 kuuawa katika shambulio la mtu kujilipua lililolaumiwa kwa kundi moja la Pakistan.