Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limemuomba Mwenyekiti wa Tume hiyo kutuma ujumbe maalumu nchini Sudan Kusini ambapo hofu imeongezeka ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Baraza limemhimiza Mwenyekiti wa Tume ya AU kupeleka ujumbe wa ngazi ya Juu nchini Sudan Kusini ili kuzishirikisha pande zote kushughulikia mzozo uliopo,” limesema Baraza hilo la AU katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wake kuhusu Sudan Kusini.
Wimbi la hivi punde la ghasia lilizuka Machi 4 wakati wanaojiita White Army - wanamgambo wa vijana - walipovamia kambi ya jeshi la Sudan Kusini huko Nasir, jimbo la Upper Nile.
Vikosi vya Serikali vilianzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya angani kwenye maeneo ya raia, kwa kutumia mabomu ya mapipa ambayo inadaiwa yalikuwa na viongeza kasi vinavyoweza kuwaka.
Baraza la Usalama la AU limesisitiza umuhimu wa Mwenyekiti wa Tume ya AU kushughulikia haraka changamoto za kitaasisi zinazoikabili ofisi ya AU nchini Sudan Kusini ili kuuwezesha maafisa wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Umoja wa Mataifa unaonyesha hofu yake kwa kile ilichokiita “mashambulizi ya kiholela katika maeneo ya Sudan Kusini.”

Wimbi la hivi punde la ghasia lilizuka tarehe 4 Machi wakati wanaojiita White Army - wanamgambo wa vijana - walipovamia kambi ya jeshi ya Sudan Kusini huko Nasir, jimbo la Upper Nile.
UN imesema Sudan Kusini inaelekea ukingoni mwa kurejea katika vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe huku ghasia zikiongezeka na mivutano ya kisiasa ikizidi.
Baraza hilo la AU pia limeihimiza serikali ya muda ya Sudan Kusini kuongeza juhudi za kuunda taasisi muhimu za nchi.
Serikali ya muda imehimizwa kukusanya rasilimali kwa vyombo vitatu vya kutunga katiba na uchaguzi, ambavyo ni: Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ya Kitaifa ya Marekebisho ya Katiba (NCRC), na Baraza la Vyama vya Siasa (PPC) ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” imesema taarifa ya AU.
Sudan Kusini iliahirisha uchaguzi wake kutoka Disemba 2025 hadi Disemba 2026 kwa madai kwamba haikuwa tayari kufanya uchaguzi.