Akiwa anafahamika kwa jina halisi la Judith Wambura Mbibo, hapana shaka Lady Jay Dee ndiye malkia wa Bongo Fleva nchini Tanzania, na pengine anaweza asitokee mwingine zaidi yake.
Gwiji huyu wa Bongo Fleva mwenye tuzo nyingi za muziki, ndani na nje ya Tanzania, alizaliwa miaka 45 iliyopita huko mkoani Shinyanga.
Hata hivyo, Lady JayDee aligeukia taaluma ya uandishi wa habari na kufanya kazi na kituo cha Clouds FM cha nchini Tanzania, kabla ya kurudi tena kwenye muziki, akishiriki kuimba wimbo maalumu wa maombolezo wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, uitwao ‘Tutakukumbuka Daima’ mwaka 1999.
Hii ni baada ya kutoka kimuziki baada ya kushinda shindano la kusaka vipaji lililokuwa likiendeshwa na kipindi cha Dj Show cha Radio One miaka hiyo.
Kwa mujibu wa Lady Jaydee mwenyewe, baada ya kushinda shindano hilo, alipelekwa kwenye studio za MJ Records kwa Master Jay ambaye alimrekodia bure na huo ndio ukawa mwanzo wa safi yake kimuziki.
Albamu yake ya kwanza kumtambulisha kwenye ulimwengu wa muziki iliitwa ‘Machozi’, ikiwa na wimbo wa machozi wenyewe ambao ulimbeba kwa muda mrefu, ukimpa jina la utani la ‘Binti Machozi’ na baadaye kubeba jina la kundi lake la muziki, Machozi Band.
Kisha zikafuata albamu za kutosha kama vile ‘Nasonga Mbele’, ‘Shukrani’, ‘The Best Of Lady Jaydee’, ‘Nasimama’, ‘Nakupenda’, ‘Siku Hazigandi’, ‘Nothing But The Truth’, ‘Woman’, ‘Binti’, ‘Moto’, ‘Siri Yangu’, ‘Ndindindi’, ‘I Love My Self’ na ‘One Time’, zenye nyimbo ambazo zilizoshika na zinaendelea kushika hadi hii leo.
Kama ulikuwa hujui, ‘Binti Komando’ ni kati ya wanamuziki wa kwanza wanawake kuimba nyimbo za R&B kwa Kiswahili.
Linapokuja suala la kufanya kolabo na wanamuziki wengine, Lady Jay Dee hakubaki nyuma.
Unakumbuka ‘Bongo Dar es Salaam’ alioufanya na Profesa Jay?
Vipi kuhusu ‘Machoni Kama Watu’ aliofanya na AY au ‘Wanonok’ alioshirikishwa na Mandojo na Domo Kaya?
Idadi ndefu ya kolabo
Alishirikishwa na Matonya kwenye wimbo ‘Anita’, ‘Nitafanya’ akiwa na Kidum, na ‘Nitampata Wapi’, alioshirikiana na Longombas kutoka Kenya.
Pia, amewahi kuimba pamoja na Oliver Mtukudzi wa Zimbabwe kwenye wimbo ‘I’m who I’m’, na kundi la Mina Nawe kutoka Afrika Kusini kupitia wimbo wa ‘Njalo-Zumba’.
‘Binti Machozi’ aliwahi kunukuliwa akisema kuwa anaheshimu sana kazi yake ya muziki na ndio sababu ya kudumu kwa muda mrefu mpaka leo.
Muziki na Biashara
Nje ya muziki, Lady Jay Dee ni mfanyabiashara anayemiliki mgawaha maarufu jijini Dar es Salaam uitwao ‘Nyumbani Lounge’ na studio iitwayo Jag Records.
Aliwahi kufunga ndoa na aliyekuwa mtangazi wa Clouds FM Garder G Habash, kabla ya wawili hao kutengana rasmi mwaka 2016.
Oktoba mwaka 2024, malkia huyu wa Bongo Fleva alituzwa kwenye ‘Bongo Fleva Honors’ kwa kutambua mchango wake kwenye muziki huo na Juni 13 mwaka huu, atafanya onesho lake la ‘Silver Concert’ maalumu kwa ajili ya kusherekea miaka 25 katika muziki.