Muda mchache baada ya kipyenga cha mwisho kuwathibitisha Liverpool kama washindi wa Ligi Kuu ya England ikiwa ni msimu wa kwanza tu wa kocha Arne Slot, Mholanzi huyo alimmwagia sifa mtu aliyemtengenezea njia ya mafanikio kwenye klabu hiyo.
Katika kusherehekea ushindi wa Ligi kuu ya England Slot aliwaongoza mashabiki wa Liverpool kumsifu kwa nyimbo kocha anayependwa zaidi Anfield, Juergen Klopp.
Baada ya mechi yake ya mwisho na Liverpool msimu uliopita, Klopp, ambaye alishinda mataji saba makubwa katika kipindi chake cha miaka tisa na timu hiyo, aliwahamasisha mashabiki Anfield kuimba wimbo huo -- uliokuwa na mahadhi ya bendi ya Austria Opus "Life is Life"
Mipango ya Klopp ilifanya kazi kuwa rahisi kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 46. "Kwa sababu ya (Klopp) ya kile alichofanya, kabla hata sijafika hapa,"
Slot alisema, alipoulizwa kwa nini anamsifia Mjerumani huyo aliyewapa Liverpool ushindi wa EPL 2020.
"Nadhani si jambo ambalo kocha yoyote amewahi kufanya hivyo, kwa hiyo hilo lilinisaidia sana.
‘Juergen anastahili sifa’
"Amenisaidia zaidi kutokana na timu ambayo ameiacha na utamaduni alioujenga wa kufanya kazi kwa bidii, siyo tu kwa wachezaji bali hata kwa benchi la ufundi umekuwa wa maana sana. Kwa sababu hizo, nimeona kuna fursa muhimu ya kumshkuru kwa kweli."
Nahodha wa Liverpool Virgil van Dijk alionekana kutokuwa na furaha baada ya mechi ya mwisho ya Klopp, akijaribu kujizuia asilie wakati akimkumbatia kocha huyo katika uwanja wa Anfield.
" Kumrithi Juergen, ni kazi kubwa sana na nadhani kocha pamoja na benchi lake la ufundi wamefanya kazi nzuri. Bila shaka anastahili sifa kwa hilo," Van Dijk alisema Jumapili.
"Sidhani kama kuna mtu yoyote -- bila shaka hilo limesemwa na watu wengi sana -- angedhani kuwa tungeshinda Ligi Kuu ya England."
Slot anakuwa kocha wa tano kushinda EPL katika msimu wake wa kwanza England, na Mholanzi wa kwanza kushinda Ligi Kuu ya England.
Itachukuwa muda kwa mimi kuzowea hali hii.
"Siamini kwa kweli, kwa sababu umelifanyia hili kazi sana, na alafu inapotokea kufanikiwa, unahitaji muda kidogo kutafakari," alisema.
‘Hii ilikuwa ya kipekee’
Alipoulizwa kuhusu hisia zake, Slot alisema "Hisia zangu zaidi zilikuwepo nilipowasili uwanjani na kuona umuhimu wa jambo hili kwa mashabiki, inamaanisha nini kwa watu hawa, na sisi kupata nafasi ya kushinda.
"Nadhani kila mtu aliyekuwa ndani ya basi alihisi hivyo, kama mashabiki wanatuunga mkono, basi haiwezekani kwetu kupoteza mechi hii."
Slot hakueleza yale ambayo mmiliki wa Liverpool John Henry alisema wakati waliposalimiana na kupongezana.
"Ilikuwa hali ya kipekee (kwa mmiliki) kuwa sehemu ya sherehe hizi na kwa wao kuniamini mimi kwa jukumu hili," Slot alisema. "Labda sasa kila mtu anasema, 'Ah, ndiyo inawezekana'. Lakini kipindi kile nakubali jukumu hili, labda siyo kila mtu alikuwa anadhani ningefanya kitu kama wanavyoamini sasa hivi.
"Kwa hiyo inaonesha namna klabu hii ilivyo ya kipekee, na kwamba siyo kila wakati wanafanya mambo ya rahisi au kile ambacho watu wanatarajia, lakini wanafanya maamuzi ambayo wanaamini ni mazuri kwa klabu."
Alipoulizwa kuhusu watakavyosherehekea Jumapili usiku na kama kutakuwa na mazoezi Jumatatu, Slot alisema "hamna" mazoezi, na "labda glasi ya pombe kidogo. Pengine mbili. Au tatu."