Tanzania: Gesi ya Helium inavyoleta nafuu ya maisha kwa wananchi
AFRIKA
4 dk kusoma
Tanzania: Gesi ya Helium inavyoleta nafuu ya maisha kwa wananchiHii ni baada ya kugundulika kwa gesi adimu ya Helium katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo.
Ugunduzi huo, ulioongozwa na kampuni ya Helium ya One Global, ulihusisha eneo la hekari zaidi ya 36, ambalo lilichukuliwa kutoka kwa wananchi wa sehemu hiyo na serikali ya Tanzania./Picha: @MadiniTanzania / Others
tokea siku moja

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, zilizopo Kusini mwa Jangwa la zilizojaliwa kuwa na rasilimali nyingi, ikiwemo madini adimu na gesi asilia.

Licha ya utajiri huo, baadhi ya watu wake, bado wanalalamika kutonufaika na rasilimali hizo.

Wakati mwingine, baadhi ya vijiji vilivyo karibu na maeneo yanapochimbwa madini hayo, hukabiliwa na ukosefu wa huduma muhimu kama vile vituo vya afya, maji na miundombinu.

Hata hivyo, nuru imeaanza kuwaangazia wakazi wa vijiji vya Itumbula, Lwate, Kamsamba, Mkonko na Muungano vilivyopo wilayani Momba, Mkoani Songwe kusini mwa Tanzania.

Hii ni baada ya kugundulika kwa gesi adimu ya Helium katika maeneo hayo.

Ugunduzi huo, ulioongozwa na kampuni ya Helium ya One Global, ulihusisha eneo la hekari zaidi ya 36, ambalo lilichukuliwa kutoka kwa wananchi wa sehemu hiyo na serikali ya Tanzania.

Kulingana na serikali ya nchi hiyo, tayari kibali kimetolewa kwa kampuni hiyo kwa eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 480 kwa ajili ya uchimbaji.

Mbali na wilaya ya Momba, mradi huo pia unahusisha sehemu ya eneo la wilaya ya Sumbawanga katika Bonde la Rukwa Kusini, huku baadhi ya wananchi wakionesha matumaini yao kupitia mradi huo.

Katika kijiji cha Kamkonko, kilichoko kilomita chache kutoka eneo la mradi, ujenzi wa wa kituo cha afya kilichoanza kuhudumia wagonjwa mwishoni mwa mwaka 2024 umekamilika.

Hatua hiyo imetoa unafuu kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita takriban 20 kufuata huduma za matibabu.

Katika mahojiano yake na TRT Afrika, Tedy Kasian ambaye alifika katika zahanati kupata matibabu, anaonesha matumaini makubwa kufuatia uwepo wa kituo hicho cha afya karibu na eneo lake.

“Kabla ya hapo hali ilikuwa mbaya, wajawazito walijifungulia majumbani,” Tedy anaeleza.

Kulingana na uongozi wa kituo hicho cha afya, kadiri muda unavyozidi kwenda, ndivyo idadi ya wagonjwa inavyoendelea kuongezeka, kutoka wagonjwa 60 kwa mwezi hadi zaidi ya watu 200.

Licha ya kutoa huduma muhimu ya afya, bado kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa.

“Hatuna umeme na vitendea kazi vingine, hivyo na tunaomba serikali itusaidie,” anasema Aneth Andrea, muuguzi mkunga mfawidhi katika kituo hicho.

Uwekezaji

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Tanzania Dkt. Nasibu Mramba ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Biashara (CBE), anasema ni wakati wa serikali ya Tanzania kuwa na mpango mkakati wa muda mrefu kwa rasilimali zake, ikijumuisha kutafuta wawekezaji watakaojenga viwanda katika maeneo husika ili wananchi wake wanufaike.

Hata hivyo, Dkt. Mramba anatilia shaka uwezo wa elimu ya wananchi juu ya umuhimu wa gesi hiyo adimu inayotumika katika huduma za afya, utafiti wa anga, na sekta ya ulinzi, kwa kile anachokiita kuwa na fikra mbaya kuhusu mustakabali wao.

“Nchi nzima ingesema madini yaliopatikana katika wilaya fulani yasichimbwe badala yake atafutwe mtu atakayejenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na madini, pengine serikali ingebadili msimamo kabisa,” anasisitiza Mramba.

Tanzania sasa inaingia miongoni mwa mataifa kadhaa, yakiwemo Marekani, Urusi, Qatar, Saudi Arabia na Algeria yanayochimba gesi ya aina hii inayotumiwa katika vifaa vya MRI, roketi na mitambo ya mawasiliano ya angani.

Kauli ya Wizara ya Madini

Akiwa jijini Dodoma, mwishoni mwa juma Waziri wa Madini nchini Tanzania Anthony Mavunde amekiri kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya mchango wa sekta ya madini kuwa mdogo ukilinganishwa na madini yanayochimbwa nchini humo.

Hata hivyo, amesema mchango wa sekta hiyo kwa pato la taifa kwa mwaka 2024 ni asilimia 10.1 kutoka asilimia 9.1 kwa mwaka 2023.

“Kumekuwa na malalamiko kwa miaka mingi kutoka kwa Watanzania kwamba mchango wa sekta hiyo kwa wananchi ni mdogo sana ikilinganishwa na rasilimali tulizojaliwa,” alisema Mavunde.

Hakuna uhakika wa lini uzalishaji utaanza, lakini tayari serikali inajadiliana na kampuni ya One Global kuhusu namna gani nchi itanufaika na gesi hiyo.

Wakati huo huo, baadhi wameanza kuonesha matumaini kwamba endapo uzalishaji utaanza basi huenda manufaa yakaonekana.

“Ni mapema kusema ni lini tutaanza uzalishaji, lakini tunatumai kuwa tutaanza mapema, kwa sababu hatuhitaji migodi mikubwa kwa uzalishaji na vitendea kazi tulivyo navyo vinatosha kuanza,” alisema Chone Malembo, Afisa Madini Mkazi Mkoani Songwe.

Kwa upande wake, msimamizi mkuu wa eneo la uchimbaji, Emanuel Ghachocha anasema kuwa utafiti utaendelea katika baadhi ya maeneo mengine nchini ili kugundua na kufanya uzalishaji wa gesi hiyo.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us