Baraza la Mawaziri la Kenya limeidhinisha Muswada wa Fedha wa 2025, ambao unalenga kuziba mianya ya kodi badala ya kuanzisha kodi mpya.
"Muswada unalenga kupunguza hatua za kuongeza ushuru," ilisoma taarifa ya Baraza la Mawaziri iliyotumwa kwa waandishi wa habari baada ya mkutano ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Serikali imesema inalenga kuimarisha mapato kupitia ufanisi wa kiutawala.
Mabadiliko muhimu ni pamoja na kurahisisha urejeshaji wa kodi, kuimarisha sheria za migogoro ya kodi, na kurekebisha sheria kuu za kodi ili kupunguza ukwepaji.
"Biashara ndogo ndogo zitaruhusiwa kupunguza gharama ya zana na vifaa kamili katika mwaka wa ununuzi," ilisema taarifa hiyo.
Mwaka wa 2024, Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2024 ambao haukupendwa na watu wengi ulisababisha ghasia kubwa zilizoongozwa na vijana, na kusababisha vifo vya watu wengi na shambulio dhidi ya Bunge, huku waandamanaji wakichoma sehemu ya jengo hilo.
Mnamo Juni 26, 2024, Rais Ruto alikataa kuidhinisha Muswada wa Fedha wa 2024.
Katika kurejelea Muswada huo ili kuchunguzwa upya na Bunge la Kitaifa, Rais alisema alizingatia maoni ya wananchi kuhusu kutoridhika kwao kwa Muswada huo.
Rais aliurudisha Mswada huo Bungeni ili kuangaliwa upya baada ya mapendekezo ya kufuta baadhi ya vifungu katika Mswada huo.
Hii ilikuwa katika kutekeleza mamlaka aliyopewa na Katiba ya Kenya 2010 katika Kifungu cha 115(1)(b).
Muswada huo ulipangwa kuanza kutumika tarehe 1 Julai 2024 baada ya kuidhinishwa na rais, na hii ilikuwa baada ya kupita kwa mafanikio katika hatua nyingine zote za mchakato wa kutunga sheria.
Hatua mpya za ushuru zilipangwa kuwa zingeanzishwa kupitia Muswada mpya wa Sheria ya Fedha au Muswada wa Marekebisho ya Ushuru ambao unapaswa kupitia mchakato wa lazima wa ushiriki wa umma kabla ya kupitishwa kuwa sheria.