Katika taarifa, wizara ya mambo ya ndani imetoa hakikisho kwa umma kuwa IPOA inachunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa polisi, licha ya watu kudhani kuwa shirika hilo limeshindwa katika kutekeleza majukumu yake ya kuwawajibisha maafisa waliokwenda kinyume na utaratibu.
“Pamoja na kuwepo kwa wasiwasi wa umma kuhusu utekelezaji wa haki ni sahihi, Kenya inaongozwa na mifumo ya sheria na utaratibu wa mahakama,” Wizara ilisema, ikiongeza, “Watu kupiga kelele mitandaoni au upendeleo wa vyombo vya habari haichukui nafasi ya mchakato wa kisheria.”
Wakenya wamelaumu bodi hiyo ya IPOA kwa kujivuta katika kuchunguza matukio ya vurugu za polisi kukabiliana na waandamanaji waliovamia bunge 25 Juni, 2024. Walioingia bunge wakati huo walikuwa wanapinga muswada wa fedha ambao walidai ulikuwa kandamizi.
Siku ya Jumatatu IPOA ilisema kuwa imepokea malalamiko 60 ya watu kuuawa wakati wa maandamano, kati ya hayo malalamiko 22 wamekamilisha uchunguzi, 36 wanayachunguza , na tayari wamewasilisha kesi mbili mahakamani.
Mamlaka zinasema mauaji mengi yalitokana na majeraha ya risasi na kupigwa na vifaa butu, ilhali mengine ni kupigwa na watu, mabomu ya machozi, kunyongwa, na kuzama kwenye maji. Katika malalamiko mawili, hakuna upasuaji wa maiti uliofanywa.
Malalamiko mengi yametoka katika mji wa Nairobi ambao ulikuwa kitovu cha maandamano. Sehemu zingine ambazo wananchi wamewasilisha kero zao kwa IPOA ni pamoja na miji ya Nyeri, Kisumu, Kakamega, Mombasa, Meru, Nakuru, na Eldoret.