FIFA imeiadhibu klabu ya ligi daraja la pili nchini Kenya kwa kupanga matokeo, na wameishusha daraja hadi ligi daraja la tatu, shirikisho la soka duniani lilisema siku ya Ijumaa.
"Kamati ya nidhamu ya FIFA pia imeagiza kushushwa daraja kwa timu ya Muhoroni Youth hadi daraja la chini katika mashindano ya soka nchini Kenya," FIFA ilisema.
FIFA imesema klabu hiyo imearifiwa kuhusu uamuzi huo na iko huru kukata rufaa.
Udanganyifu katika ligi
Mchezo wa soka nchini Kenya umekumbwa na matukio ya kupanga mechi katika kipindi cha hivi karibuni huku shirikisho la soka la Kenya FKF likiwasimamisha wachezaji 14 na makocha wawili tangu Januari 2023 kufuatia taarifa za udanganyifu katika ligi ya nyumbani.
Mwezi Februari 2020, FIFA iliwapiga marufuku ya maisha wachezaji wanne wanaocheza ligi ya nyumbani kwa kuhusika na "mtandao wa kimataifa" katika kupanga matokeo ya ligi.
Baadaye waamuzi watano wa Kenya pia walitimuliwa kufuatia sakata hilo.