Uzalishaji wa madini ya shaba nchini Zambia umeongezeka kwa hadi 30% katika kipindi cha robo ya kwanza ya 2025, kufikia tani 224,000 ikilinganishwa na tani 173,000 katika kipindi kama hicho 2024, Waziri wa Madini Paul Kabuswe amesema.
Katika taarifa siku ya Jumatano, Kabuswe alisema uzalishaji mkubwa wa makampuni mawili makubwa, Konkola na Mopani, ulichangia kuongeza kiwango hicho kwa ujumla.
Mwezi Januari, Zambia ilitangaza kuwa uzalishaji wa shaba umeongezeka kwa 12% mwaka 2024, kutokana na kuimarika kwa uzalishaji katika migodi muhimu huku serikali ikiweka matumaini katika sekta hiyo kukuza uchumi wa nchi.
Sasa imefika karibu tani 820,670 kutoka tani 732,580 mwaka 2023, alisema Kabuswe wakati huo.
Mamlaka zinasema uzalishaji wa madini ya shaba umepanda licha ya kuwepo kwa mgao wa umeme baada ya ukame uliotatiza katika kituo cha kuzalisha umeme.
Zambia ni ya pili barani Afrika kwa kuzalisha madini ya shaba baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,na serikali ina lengo la kufikia kiwango cha tani milioni 3 kwa mwaka katika kipindi cha muongo mmoja ujao.