AFRIKA
3 dk kusoma
Afrika yaadhimisha wiki ya chanjo wataalam wakihimiza uwekezaji zaidi
Takwimu zinaonyesha kuwa Afrika inachangia asilimia 58 ya vifo duniani kutokana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Afrika yaadhimisha wiki ya chanjo wataalam wakihimiza uwekezaji zaidi
Siku ya chanjo katika kituo cha Afya cha Katooke 3 katika WILAYA ya Mukono, Uganda/ picha Gavi / Public domain
tokea masaa 20

Huku dunia ikiadhimisha wiki ya chanjo kituo cha afya cha Afrika, Africa CDC kinatoa wito kwa nchi barani kuwekeza zaidi katika mpango wa kutoa chanjo kwa ajili ya kukinga na kutibu magonjwa.

“Kila mwaka, Afrika inachangia asilimia 58 ya vifo duniani kutokana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Hili sio tu shida ya kiafya, ni suala la haki na usawa,” Africa CDC imesema katika ujumbe wake mtandaoni.

Africa CDC inasema Afrika inaweza kuongoza njia katika upatikanaji wa chanjo, lakini tu ikiwa itawekeza katika mifumo ya afya na umiliki wa ndani.

“Kwa kuimarisha mifumo yetu ya kitaifa na ushirikiano wa bara, tunaweza kuhakikisha kwamba chanjo inasalia kuwa kipaumbele cha kwanza na kwamba kila mtoto anapata ulinzi anaostahili. Hebu tufanye chanjo kuwa kipaumbele-sio tu wiki hii, lakini daima,” imesema.

Maendeleo kwa chanjo

Takwimu zinaonyesha kuwa mnamo 2023, chanjo iliokoa maisha ya watu milioni 1.8 katika kanda ya Afrika, karibu nusu ya idadi ya watu milioni 4.2 ulimwenguni.

Takwimu zinaonyesha Afrika pia imepata maendeleo makubwa katika vita dhidi ya polio, ikirekodi kupungua kwa 93% kwa maambukizi aina 1 ya virusi vya polio kutoka 2023 hadi 2024 na kupungua kwa 65% kwa maambukizi aina ya 1 ya virusi vya polio katika mwaka uliopita.

Zaidi ya watoto milioni 5 wa ‘dozi sifuri’ - watoto ambao hawajapata dozi moja ya chanjo muhimu ya kawaida barani Afrika - wamechanjwa tangu 2024 katika kampeni iliyowekwa katika nchi 20 za kipaumbele.

Wasichana wengi kuliko hapo awali wanalindwa dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, ugonjwa ambao huua mwanamke kila baada ya dakika mbili duniani kote.

Wataalam wanasema chanjo ya Human Papillomavirus (HPV) (dozi moja) imeongezeka hadi 40% mwaka 2023 kutoka 28% mwaka uliopita - na kuifanya Afrika kuwa eneo la pili kwa kiwango cha juu cha chanjo duniani, kuwezesha mamilioni ya wasichana kutimiza uwezo wao.

Mwaka huu, Wiki ya Chanjo Duniani na Wiki ya Chanjo ya Afrika ambayo inaadhimishwa chini ya kaulimbiu, “Chanjo kwa Wote Inawezekana Kibinadamu, inalenga kukuza nguvu ya kuokoa maisha ya chanjo ili kuwalinda watu wa rika zote dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Changamoto za ufikiaji wa chanjo

"Tumepiga hatua kubwa katika kupanua chanjo na kuokoa maisha, kutokana na kujitolea kwa serikali na washirika. Lakini bado tuna msingi zaidi wa kufunika. Lazima tuendeleze na kupanua juhudi hizi za kuokoa maisha ili kujenga mustakabali wenye nguvu na afya kwa wote," alisema Dkt. Chikwe Ihekweazu, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la afya Duniani, WHO Kanda ya Afrika.

Maendeleo haya yamewezekana kutokana na juhudi za serikali na usaidizi kutoka kwa washirika ikiwa ni pamoja na Gavi, Muungano wa Chanjo (Gavi), UNICEF, Shirika la Afya Duniani (WHO) na wengine.

Gavi, kati ya wazalishaji mkubwa wa chanjo duniani inasema changamoto bado zinaendelea katika kuwafikia watoto wengi barani.

“Mtoto mmoja kati ya wanne hubakia bila chanjo au kukosa chanjo muhimu za kawaida na mtoto mmoja kati ya watano hajachanjwa, huku nchi nyingi zikikabiliwa na milipuko ya mara kwa mara, hasa ya surua - ugonjwa unaoambukiza sana na unaoweza kusababisha kifo,” Gavi imesema katika taarifa.

Inasema mapengo haya ambayo yanaacha eneo hilo katika mazingira magumu, yanaweza kuhusishwa na vikwazo pamoja na upatikanaji mdogo wa huduma za afya katika maeneo ya mbali mara nyingi kutokana na migogoro na kukosekana kwa utulivu.

Pia kuna vikwazo vya vifaa na usafirishaji, wananchi wengine kusita kupata chanjo kutokana na taarifa potofu, na uhaba wa fedha kwa ajili ya mipango ya chanjo. Inasema changamoto hizi zinachangiwa zaidi na usumbufu unaosababishwa na dharura za afya ya umma.


CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us