Kulikuwa na tumaini la kupatikana kwa amani nchini Sudan hasa baada ya mamilioni ya watu katika taifa hilo kujikuta katikati mapigano, ukame na magonjwa.
Mwenendo wa vita hivyo umebadilika, hasa baada ya kudhibiti maeneo muhimu ikiwemo uwanja wa ndege, benki kuu na ikulu ya rais.
Mwezi Machi mwaka 2025, Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, alirudi kwenye kitu cha uongozi wa nchi hiyo, kwa mara ya kwanza toka Aprili 15, 2023.
“Kuna tumaini kidogo bado sehemu kubwa ya nchi haina utulivu,” anasema Davis Makori, kutoka Shirika la PLAN International, katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Mgogoro wa Sudan ulianza baada ya Jenerali Fattah al-Burhan kutofautiana na aliyekuwa makamu wake, Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti ambaye anaongoza kikundi cha RSF.
Kikundi cha RSF kimezidi kufanya mashambulizi katika eneo la Darfur, hasa baada ya kutimuliwa kutoka Khartoum.
Zaidi ya watu 300 wameripotiwa kuuwawa kuanzia Aprili 11.
“Watu wa katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam wanazidi kushambuliwa,” anasema Marion Ramstein, mratibu wa dharura kutoka shirika la MSF, kaskazini mwa Darfur.
“Zipo taarifa za watu kukimbilia maeneo tofauti, japo hatuna takwimu sahihi kwa sasa.”
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa jeshi la Sudan," anasema Pascal Cuttat, mshauri mwandamizi kutoka taasisi ya Sahan iliyopo nchini Kenya.
Watoto vitani
Kumekuwepo na janga kubwa la kibinadamu nchini Sudan, wakati machafuko yakiingia mwaka wa tatu.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milioni 15, ambayo ni ni theluthi moja ya idadi ya watu wa Sudan, wameyakimbia makazi huku wengine 24,000 wakiuwawa.
Wakati huo huo, matukio yanahusika na unyanyasaji wa kijinsia yameongezeka nchini humo , huku watoto na wanawake wapatao milioni 12.1 wakiwa katika mazingira hatarishi.
“Kutakuwa na athari kubwa za kisaikolojia kwa watoto hata kama vita hivi vitamalizika kesho,” anaeleza Makori.
“Sio tu kutelekezwa na kunyanyaswa, watoto hawa wamepoteza marafiki na haki yao ya kupata elimu.”
Katika kuwaondolea kadhia hiyo, mashirika mbalimbali kama vile Plan International wameandaa majukwaa rafiki kwao, yatakayowapa fursa ya kukutana na kucheza pamoja na marafiki zao.
“Waliweza kuzoeana japo walikuwa waoga katika siku ya kwanza,” mwezeshaji kutoka Plan International, Nasra Abdalla anaiambia TRT Afrika.
Asma(si jina lake halisi), ameponea kadhia hiyo toka akimbie makazi yake mjini Khartoum akiwa na watoto wake, miezi 22 iliyopita.
Alitekwa na kikundi cha wanaume, katika shamba moja la ndizi, lililo karibu na eneo ambalo alijihifadhi, akiwatafutia watoto wake chakula.
“Nilijaribu kuwaambia kuwa walikuwa sawa na watoto wangu,” Asma anasema. “Wakafanya wanalolijua, nikaanza kuhara, sijui ni kama ni kutokana na kile walichonifanyia.”
Huku sekta ya afya ikiwa imeelemewa kutokana na machafuko hayo, ilimlazimu Asma kuendelea kutafuta sehemu salama yeye pamoja na watoto wake.
“Nilipofika kambini, nikakutana na msaada kutoka PLAN International. Niliwaomba wanitibu ila wasimwambie mtu kile kilichonitokea,” alisema Asma, ambaye ni mama watano.
“Sipendi kusimulia kile kilichonitokea japo siwezi kuukimbia ukweli iwapo nahitaji matibabu.”
Kwa sasa Asma, ana matumaini kuwa siku moja vita hivyo vitafikia kikomo.