Umuhimu wa Moshi katika uchaguzi wa Papa mpya
Umuhimu wa Moshi katika uchaguzi wa Papa mpya
Kwa sasa macho yote yako katika bomba la moshi la Vatican kuona moshi mweupe wa kumkaribisha Papa wa 267 utatoka baada ya muda gani?
5 Mei 2025

Mchakato wa kumchagua Papa mpya wa Kanisa Katoliki umekaribia.
Katika mji wa Vatican, bomba la moshi limewekwa kwenye kanisa la Sistine, ambalo ni kiashiria kikubwa kuwa Kanisa Katoliki liko tayari kwa uchaguzi Mei 7, 2025.

Bomba hili katika historia ya kanisa limetumika kutangaza matokeo ya kura, ambapo makadinali hujifungia na kuendeleza upigaji kura usiri mkubwa.

Vatican imethibitisha makadinali 133 watashiriki katika mchakato wa kupiga kura, hivyo mshindi atahitajika kupata angalau kura 89 ambayo ni thuluthi tatu ya kura. Kenya na Uhispania zimejiondoa katika kupiga kura.

Kadinali wa Italia Fernando Filoni, afisa wa zamani wa Vaticani aliyeshiriki katika kongamano lake la pili, amesema kwamba anatarajia kura za kwanza zisiwe na maamuzi.

"Kura za awamu mbili za kwanza ni za mwelekeo, kisha tunaanza kujumlisha mambo," alisema.

Inaripotiwa kwamba, Kadinali John Njue wa Kenya hataweza kusafiri kwenda Roma kutokana na afya yake kutokuwa sawa.

Umuhimu wa moshi
Ikiwa baada ya makadinali kupiga kura hakuna atakayepata mahitaji ya theluthi tatu ya kura basi , karatasi hizo zitachomwa, kemikali maalumu itaongezwa ambayo itatoa moshi mweusi.

Ikiwa mgombea atapata kura 89 basi, kemikali itaongezwa katika karatasi hizo za kura kuchomwa na moshi mweupe utaonekana katika bomba hilo, kutangaza papa amepatikana.

Kura ya kwanza itapigwa Jumatano, Mei 7, jioni. Katika siku zinazofuata, wapiga kura wa Kardinali watapiga kura mara nne kwa siku, mara mbili asubuhi na mara mbili alasiri.

"Tunapopiga kura, hatuzungumzi, lakini baadaye tunakula pamoja, tunaishi pamoja, na kulinganisha mawazo," Kadinali wa Italia Filoni ameongezea.

Katika historia ya kanisa uchaguzi mrefu zaidi wa Papa ulikuwa katika karne ya 13, ilichukua siku 1,006. Katika mkutano uliomchagua marehemu Papa Francis 2013, mkutano ulidumu saa 27; mnamo 2005 ilikuwa masaa 26. Uchaguzi wa 1903 ulichukua siku tano.

Kwa sasa macho yote yako kwa bomba la moshi la Vatican kuona moshi mweupe kumkaribisha papa wa 267 utatoka baada ya muda gani?

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us