Rais Ruto wa Kenya ametoa msamaha kwa wafungwa 57 kutoka gerezani.
Kati yao 56 ni raia wa Kenya na mmoja raia wa kigeni.
Ikulu imesema hatua ya kuonesha huruma inalenga kuimarisha mfumo wa urekebishaji na haki.
Tangazo hilo lililotolewa Jumatatu na Ofisi ya Rais, inatokana na mapendekezo ya Kamati ya Ushauri kuhusu msamaha (POMAC) na msingi wake ni mamlaka ya kikatiba chini ya Kifungu cha 133.
Miongoni mwa waliosamehewa, 31 walikuwa wamehukumiwa vifungo vya maisha na wameruhusiwa kuwa huru lakini kwa masharti.
Aidha, raia wa kigeni kutoka nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambaye alikuwa alihukumiwa kukaa gerezani maisha amesamehewa kwa masharti na kurejeshwa nyumbani kwao.
Ofisi ya Rais imesema watu wengine 25 wataachiliwa baada ya kubadilishwa sehemu ya vifungo vyao vilivyobakia.
Rais Ruto ametangaza msamaha huo kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na msongamano wa wafungwa na kupunguza mzigo wa makosa madogo kwenye mfumo wa haki za makosa ya jinai.
Pamoja na msamaha huo, aliagiza msamaha wa jumla kwa wale waliofungwa kwa miezi sita au chini ya muda huo kwa makosa madogo, pamoja na wafungwa ambao wamebakisha chini ya miezi sita katika vifungo vyao.