Siku ya Wakunga: Mashujaa wasiotambuliwa katika  usimamizi wa masuala ya uzazi
AFRIKA
4 dk kusoma
Siku ya Wakunga: Mashujaa wasiotambuliwa katika usimamizi wa masuala ya uzaziWakunga bado ni watu muhimu katika mzunguko wa huduma za uzazi barani Afrika licha ya kutotambuliwa rasmi, kupata mafunzo, na kupewa vitendea kazi pamoja na kutokuwa na mazingira bora ya kazi.
Olga Hope Mavoungou anatoa mafunzo na kusimamia wanafunzi wa matibabu katika vyuo vikuu katika mji mkuu wa Gabon, kusaidia kuunda kizazi kijacho cha wataalamu./TRT Afrika
5 Mei 2025

Miaka mingi kabla ya utaalamu wa matibabu ya kisasa kuenea, wakunga walikuwa nguzo muhimu, wakitumia busara za jadi na umakini kuhakikisha wazazi wanajifungua salama.

Kuanzia kwa Eileithyia – aliyeheshimiwa katika hadithi za Kigiriki kama mungu wa kike aliyepunguza maumivu ya kujifungua – hadi kwa wakunga wa jadi wa Afrika, ukunga umekuwa sehemu muhimu ya mzunguko wa maisha.

Hata hivyo, ni wachache wetu wanaokumbuka mikono ilyotubeba kabla ya mama zetu wazazi kutupokea.

Hii ni hali ambayo wakunga wameizoea. Lakini jambo gumu zaidi kuelewa, na hata kukubaliana nalo, ni ukosefu wa vitendea kazi, kinga, na heshima kwa taaluma ambayo inaendelea kuwa na jukumu muhimu katika kupunguza vifo wakati wa kujifungua.

Tarehe 5 Mei ni Siku ya Kimataifa ya Wakunga, iliyoanzishwa na Shirika la Afya Duniani miaka 33 iliyopita ili kuwaenzi mamilioni ya wataalamu duniani kote – miongoni mwao Annick Nonohou kutoka Benin na Olga Hope Mavoungou kutoka Gabon, wote wakiwa na uzoefu wa miongo kadhaa katika taaluma hii.

Shauku ya Annick na Olga kwa ukunga imewafanya waendelee kujitolea katika taaluma hii licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Wote wawili wanaamini kuwa katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo zao, kunahitajika uimarishwaji wa haraka ikiwa lengo ni kuondoa kabisa vifo vya wakati wa kujifungua.

“Ukunga ni taaluma ya matibabu yenye ujuzi ulioainishwa wazi, inayodhibitiwa na vyombo vya kisheria vya kitaifa na kimataifa. Wakunga wa Afrika wangeweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ikiwa wangepata mafunzo sahihi, vifaa, msaada, na ulinzi wa kisheria,” Annick, anayefanya kazi Abomey-Calavi, anaiambia TRT Afrika.

“Katika baadhi ya nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa, wakunga wanafanya kazi chini ya kanuni zilizopitwa na wakati ambazo haziendani na sayansi ilivyo kwa sasa na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani WHO kwa lengo la kujifungua salama,” anaeleza.

Kutokwenda na wakati

Tafiti mbalimbali za WHO na mashirika mengine zinaonesha ukosefu wa mafunzo, kutokuwepo kwa huduma bora, na uhaba wa wakunga wenye ujuzi kama baadhi ya sababu kuu za vifo vya akina mama na watoto wachanga duniani.

Takwimu za vifo wakati wa kujifungua Kusini mwa Jangwa la Sahara – ni vifo 1,000 kwa kila watu 100,000 wanaojifungua – zinaonesha hali mbaya. Ikiwa si mtoto, basi ni mama, au wote wawili, wanakabiliwa na hatari kwa maisha yao wakati wa kujifungua.

Olga, anayefanya kazi ya ukunga katika Hospitali ya Libreville, anakubaliana na wasiwasi wa mwenzake kutoka Benin kuhusu umuhimu wa vifaa vya matibabu na miundombinu pamoja na mafunzo.

“Tunahitaji mazingira ya kazi yanayoturuhusu kufanya kazi zetu kwa usalama na ufanisi. Ili kuimarisha utendaji wetu na kupunguza vifo, tunatakiwa kuimarisha vituo vya huduma ya watoto wachanga na kuviwezesha kwa teknolojia inayohitajika.

Pia tunahitaji kuhakikisha kuwa kina mama na watoto wanapata huduma kwa njia ya kistaarabu na kwa kuwaonea huruma katika maeneo yaliyotengenezwa vizuri,” anasema.

Anapokuwa hafanyi kazi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Libreville, Olga hufundisha na kusimamia wanafunzi wa udaktari katika vyuo vikuu vya mji mkuu wa Gabon, akisaidia kuandaa kizazi kijacho cha wataalamu.

Heshima na ushirikiano

Pamoja na vitendea kazi, wakunga barani Afrika wanataka kutambuliwa kwa nafasi yao muhimu katika afya ya uzazi na kusaidia maisha ya watoto wachanga.

Kwa Annick na Olga, heshima ya pande zote na ushirikiano kati ya wakunga na wataalamu wengine wa afya ni muhimu kwa ufanisi wa kazi na ustawi wao wa kiakili.

“Wakunga ni kiungo muhimu kati ya kina mama na uzazi wa salama, lakini taaluma hii mara nyingi hukosa kutambuliwa na kuheshimiwa. Tunahitaji ushirikiano imara miongoni mwa wahudumu wa afya ili kupata matokeo mazuri,” anasema Olga.

Wakiwa na nia ya kuleta mabadiliko, wanawake hawa wawili wanatoa utaalamu na uzoefu wao kwa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali na vyama vingine, wakitetea uhamasishaji, mafunzo bora, na mazingira mazuri ya kazi kwa wakunga kote barani Afrika.

Lengo lao ni kuimarisha mafunzo, kuinua taaluma, na kuziba pengo la ukunga ambalo bado lipo katika nchi nyingi za Afrika.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us