Msanii Fik Gaza wa Uganda ajikuta ndani ya ‘sakata la wizi’
Msanii Fik Gaza wa Uganda ajikuta ndani ya ‘sakata la wizi’
Sakata hilo linafuatia baada ya msako wa polisi uliofanyika nyumbani kwa msanii huyo.
10 Aprili 2025

Tasnia ya muziki nchini Uganda, ilipigwa bumbuwazi kufuatia kukamatwa kwa msanii Shafik Jjingo, anayefahamika zaidi na mashabiki wake kama Fik Gaza.

Kulingana na vyombo vya habari nchini Uganda, jeshi la polisi nchini humo linaendelea kumshikilia msanii huyo.

Hata hivyo, kabla ya kukamatwa kwake, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Fiz alikana madai ya kuhusika na wizi, na kuwa alikuwa“amebambikiwa tu kesi hiyo” na watu waliokuwa na nia mbaya dhidi yake.

“Nimetaarifiwa kuwa natakiwa nikamatwe kwa kesi ya uongo! Ni wazi kuwa kuna mtu anataka kunihujumu. Sitokubali hicho kitokee!” alisema Fiz kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Madai ya uporaji

Sakata hilo linafuatia baada ya operesheni ya polisi iliyofanyika katika nyumba ya msanii huyo iiyopo katika eneo la Makindye.

Kulingana na jeshi la polisi na nchi hiyo, baada ya majadiliano na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma, msanii huyo atakabiliwa na shitaka la uporaji.

Hata hivyo, msanii huyo ameendelea kusisitiza kuwa hana hatia yoyote.

"Sitaogopa, nitasimamia ukweli," alisema.

Kwa sasa, msanii huyo pamoja na washitakiwa wenzake wako katika mahabusu ya kituo cha polisi cha Katwe, wakisubiria uchunguzi, pamoja na kufikishwa mahakamani.

‘Msanii anayechipukia’

Changamoto hiyo imetia doa kwenye safari ya kimuziki ya msanii huyo, kwani amekuwa akijizoelea umaarufu siku hadi siku kwenye tasnia ya muziki nchini Uganda.

Mwaka 2024, msanii huyo aliwania tuzo mbalimbali ikiwemo ya Galaxy FM Zzina.

Wimbo wake wa “Banana remix”, alioshirikiana na Jose Chameleone uliorodheshwa kati ya nyimbo zinazowania tuzo ya wimbo bora wa Dancehall.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us