Kukithiri kwa ukosefu wa usalama nchini Nigeria ambapo kumesababisha vifo vya watu na utekaji kwa ajili ya kutaka kikombozi, kunaendelea kuzua wasiwasi miongoni mwa raia na mamlaka.
Huku makundi ya kigaidi kama vile Boko Haram na ISWAP yakiendeleza mauaji kaskazini mashariki mwa nchi, makundi ya utekaji nyara yanaendelea kuteka watu kwa lengo la kupata kikombozi katika maeneo ya barabara kuu kwenye baadhi ya sehemu nchini. Hali hii ya ukosefu wa usalama imeendelea kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kuongezeka kwa machafuko kumesababisha Rais Bola Ahmed Tinubu kutoa agizo akisema "Sasa imetosha". Aliagiza vyombo vya usalama kujitahidi zaidi na kutaka kufanyike mabadiliko ya kimkakati ndani ya vyombo hivyo.
Matokeo ya mkutano wa hivi majuzi wa Magavana wa Nigeria (NGF), jukwaa la magavana wa majimbo 36 ya nchi hiyo, na kujitolea kufanya kazi na taasisi za serikali kuu pamoja na kutumia teknolojia, yamekwenda sanjari na kile ambacho taifa linataka katika kupata amani ya kudumu.
Agizo hilo na dhamira ya magavana, ni miongoni mwa mfululizo wa kauli za rais na juhudi zenye lengo la kuimarisha usalama wa nchi.
Swali ni: Kauli na juhudi hizi zinawezaje kuleta mabadiliko ya kuwepo kwa usalama?
Magavana kujitolea kushirikiana na serikali kuu kwa kutumia teknolojia na ubunifu inaonesha namna gani masuala magumu ya kiusalama yanavyohitaji watu kutafuta suluhu kwa pamoja. Ushirikiano huu ni muhimu, lakini lazima ufuatwe na hatua madhubuti na uwajibikaji.
Na wakati tukiangazia mbele, umakini na mkakati mahsusi unahitajika katika kutatua tatizo la machafuko sehemu mbalimbali nchini Nigeria. Lazima tuwe makini dhidi ya:
• Namna ya kutafsiri matukio: Maafisa wetu wa usalama lazima walindwe kutokana na shinikizo za watu au makundi yanayotafsiri matukio namna wanavyotaka wao, licha ya kuwafahamu wanaochochea mapigano. Hatua kama hii inaweza kusababisha matumizi mabaya ya raslimali na kuzidisha machafuko.
• Kubagua na kunyanyapaa: Utaratibu wa kubagua na kunyanyapaa baadhi ya jamii au makundi kutokana na yanayofanywa na wachache siyo tu ukiukwaji wa haki za msingi lakini pia inachochea kutengwa kwa kundi la watu na kufanya kuwepo kwa itikadi mbaya katika mizozo ya aina yote.
• Taarifa muhimu za kijasusi bila upendeleo: Msisitizo katika umuhimu wa kutumia teknolojia katika kupata taarifa za kijasusi mahsusi na zenye malengo maalum na siyo kuangazia kwa ujumla na kubagua, kuhakikisha kuwa watu wanakabiliwa inavyotakiwa na kwa uhakika, bila kuangalia chanzo cha vurugu.
Kuwa na taifa la Nigeria ambalo liko salama kunahitaji ushirikiano, ubunifu, kuimarisha mchango wa bunge, kujumuisha raia kupitia elimu na kujitolea, na dhamira ya uhakika katika kuhakikisha suluhu yenye usawa na haki kwa machafuko aina yote.
Raia wa Nigeria waruhusiwe kufanya majadiliano kuhusu vipi kwa pamoja wanaweza kufikia malengo ya usalama, haki, na mustakabali wenye uwajibikaji, ambapo mawazo ya kila mtu ni muhimu.
Maafisa wa serikali katika ngazi ya majimbo, ikiwemo magavana na wenyeviti wa serikali za mitaa, wana jukumu kubwa la kujenga msingi thabiti, ikiwa ni pamoja na miundombinu na namna ya kushughulikia kwa haraka masuala ya usalama wa umma katika maeneo ya mashinani.
Hili linahitaji mtazamo thabiti katika masuala sita muhimu:
1. Kuwepo na mtandao wa kiintelijensia na kuimarisha polisi jamii ili iwe rahisi kutambua hatari mapema
2. Kutekeleza mikakati ya usalama na miradi ya kijamii ambayo itafanya iwe vigumu kwa uhalifu na vurugu kufanyika.
3. Kuwekeza katika vituo vya kuratibu na kusimamia, huku kukiwa na mifumo ya mawasiliano ya haraka na maafisa wa usalama wa eneo ili kupunguza kufanyika kwa matukio ya utovu wa usalama
4. Kuwapa vifaa na mafunzo wahudumu wa dharura na kufanya iwe rahisi kwa vyombo mbalimbali kushirikiana kwa haraka inapotokea hali ya hatari.
5. Kuwepo na mipango ya kufanyia tathmini ya mara kwa mara mikakati na ili kutambua udhaifu na kushughulikia mbinu ambazo zinaweza kutumika.
6. Kuwa na njia ya kuwasaidia wanaopatwa na matatizo pamoja na mipango ya jamii kutafuta suluhu ya kuimarisha usalama na kuleta uthabiti wa muda mrefu.
Kuhakikisha kuwa agizo la Rais Tinubu la "Sasa imetosha", na maagizo mengine yoyote yatakayokuja, na dhamira ya magavana katika upatikanaji wa matokeo, lazima sote tuyape masuala haya kipaumbele:
Kuimarisha taasisi ya uongozi: Maafisa wanaomzunguka Rais, ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mshauri wa masuala ya Usalama pamoja na Mawaziri wa Ulinzi,Mambo ya ndani na Polisi, lazima wachukue maamuzi thabiti.
Lazima maagizo yao yawe mahsusi, yafanyiwe kazi, ikiwemo miongozo ya wazi, itifaki, na uwajibikaji. Hili litahakikisha utekelezaji usio na wasiwasi na kuepuka kauli zenye malengo mazuri kupotea bila kufanyiwa kazi.
Kuimarisha mifumo ya uwajibikaji: Hatua za uwajibikaji ni lazima, hazina mjadala. Kuwepo na taasisi huru za kufanya uchunguzi, kuimarishwa kwa taratibu za ndani za nidhamu,na uwazi katika operesheni za usalama ni muhimu kuhakikishia umma na kuwepo kwa utawala wa sheria.
Hii ni muhimu katika mazingira ambayo maagizo yaliyopita hayakutekelezwa wala watu kuwajibishwa.
Kufanya tathmini: Kuwepo na tathmini ya mara kwa mara, kwa kuzingatia takwimu. Serikali na wadau wengine lazima wafuatilie matukio ya ukosefu wa usalama, wadadavue mienendo, na kuvifahamisha vyombo vya usalama na watunga sera kuhusu wanachotakiwa kufanya. Hili linatoa fursa ya kurekebisha makosa na kuhakikisha kuwa mikakati inapigwa msasa kila wakati kwa lengo la kupata ufanisi zaidi.
Usimamizi wa bunge: Bunge lazima liwe linakagua bajeti za usalama na operesheni zake, kuhakikisha kuwa zinazingatia sheria, na kutunga sheria zinazoendana na hali ya kisasa ya usalama. Kazi hii ya bunge ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji.
Utumiaji mzuri wa teknolojia: Pamoja na kuwa wazo la magavana la kutumia teknolojia ni zuri, lazima tutoe kipaumbele kwa matumizi yake kwa kutumia maadili na kwa njia sahihi. Kukusanya taarifa za kijasusi kwa malengo mahsusi na kuacha kunyanyapaa watu ni muhimu sana.
Kuwashirikisha wananchi: Kuwekeza katika kuelimisha jamii na kusaidia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutawapa uwezo wananchi wa kushiriki katika juhudi za kutafuta amani na kuwajibisha taasisi za serikali.
Agizo la "Sasa imetosha" na dhamira ya magavana linatoa fursa nzuri. Hata hivyo, kufanikiwa kwao kunategemea zaidi uwezo wetu wa pamoja wa kuacha kuongea na kwenda katika hatua ya utekelezaji na vitendo.
Kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuimarisha uwajibikaji, kutumia vyema teknolojia, na kuwashirikisha wananchi, tunaweza kubadili maagizo ya rais na kupata mafanikio katika kuwa na usalama pamoja na kujenga Nigeria iliyo na amani na yenye ufanisi.
Mwandishi, Dkt. Kabir Adamu ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ‘Beacon Security and Intelligence Limited’, ambayo inashughulika na masuala ya usimamizi wa usalama Afrika Magharibi na maeneo ya Sahel.
Kanusho: Maoni ya mwandishi hayaakisi maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.